Saturday, June 24, 2017

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWATAKA TRA WASIWATOZE KODI YA MAJENGO WAZEE WENYE UMRI WA MIAKA 60

Na Mwandishi maalum,
Chato.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka maafisa wa Mamlaka ya Mapato hapa nchini (TRA) wakusanye kodi za majengo kwa kuzingatia sheria na wasiwatoze kodi ya majengo Wazee wenye umri zaidi ya miaka 60.

Alitoa agizo hilo juzi wakati alipokuwa akizungumza na wananchi na viongozi wa wilaya ya Chato mkoa wa Geita ambao walihudhuria uzinduzi wa jengo la Mamlaka ya mapato wilayani humo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

“TRA ijipange upya namna ya kukusanya kodi za majengo kuanzia Julai Mosi mwaka huu, katika kutekeleza jukumu hili zingatieni sheria na taratibu husika zilizowekwa tusisikie mnawadai kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 kwa majengo ambayo wanayatumia kama makazi yao,” alisisitiza Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka pia maafisa hao wakusanye kodi ya majengo kwenye maeneo ya mjini na siyo vijijini kwani kodi hiyo haiwahusu.


“Msiende vijijini ambako kuna nyumba za nyasi au za tembe hazihusiki tembeleeni nyumba za mijini, piteni kwenye mitaa muainishe aina zote za nyumba zinazostahili kulipiwa kodi mkishafanya sensa, wekeni utaratibu wa kuwawezesha wananchi kulipia kodi hizo”, alisema.

Pia aliwataka wananchi wanaonunua bidhaa wanapaswa kudai risiti mara wanunuapo bidhaa hizo, lakini wahakikishe wanapewa risiti yenye kiwango halisi walicholipia.

Vilevile awali akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja la TRA mkoani humo Kamishna mkuu wa TRA, Charles Kicheere alisema ujenzi huo ulianza Julai 12 mwaka jana na kukamilika ujenzi wake Juni 12 mwaka huu.


Kicheere aliongeza kuwa ujenzi wa jengo hilo umegharimu shilingi bilioni 1.4 na kwamba ulichochewa na ongezeko kubwa la idadi ya walipakodi wilayani Chato kutoka watu 150 mwaka 2010 hadi 2011 na kufikia watu 600 mwaka jana na mwaka huu.

No comments: