Wednesday, June 7, 2017

SERIKALI MKOANI RUVUMA YAJIWEKEA MKAKATI WILAYA YA NYASA KUWA KIVUTIO CHA UTALII NA UWEKEZAJI


Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge upande wa kulia, akizungumza juzi na vijana ambao aliwakuta wakiosha pikipiki zao kandokando ya ziwa Nyasa wilayani Nyasa mkoani humo ambapo alisema, shughuli hizo zinatajwa kuchangia kuadimika kwa samaki katika ziwa hilo kwani mafuta yanayotoka kwenye vyombo hivyo ni sumu na husababisha viumbe hai waliopo kwenye ziwa hilo kama vile samaki na viumbe wengine kupoteza uhai wao.(Picha na Muhidin Amri)
Na Mwandishi wetu,
Nyasa.

KUFUATIA uwepo wa samaki wengi wa mapambo katika ziwa Nyasa mkoani Ruvuma, serikali imejiwekea mkakati wa kuifanya wilaya ya Nyasa mkoani humo kuwa ndiyo kivutio cha utalii na uwekezaji, kutokana na wilaya hiyo kuwa katika mazingira mazuri yanayovutia watalii wa kutoka ndani na nje ya maeneo mbalimbali wilayani hapa.

Uwepo wa sifa hizo katika ziwa hilo, linatajwa pia kuwa na samaki wa mapambo zaidi ya 320 ambao wengine hutumika kwa kitoweo cha binadamu.

Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa akizungumza na Wananchi wa kata ya Mbamba bay na Wadau  wa mazingira wilayani Nyasa, wakati akiongoza shughuli za usafi  wa mazingira katika maeneo mbalimbali.

Dkt. Mahenge alisema kuwa kutokana na baadhi ya wananchi wamekuwa wakionekana kutofahamu umuhimu wa ziwa hilo, jambo hilo limekuwa likichangia na kusababisha kukwamisha mkakati wa maendeleo ya utangazaji wa vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo.


Hivyo basi, aliwataka viongozi wa wilaya kwa ujumla kuhakikisha kwamba wanaweka mkakati kabambe na endelevu katika suala zima la usafi wa mazingira kwenye maeneo yote na kutolifanya suala hilo kuwa la kisiasa.

Alisema kuwa hataweza kufanikiwa mkakati wa kuifanya wilaya ya Nyasa inakuwa na kituo cha vivutio vya utalii na uwekezaji, endapo hakutakuwa na mazingira mazuri yanayoshawishi watu kwenda na kupenda kuwekeza katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Bila kuwa na mazingira rafiki ni vigumu kwa mkoa kufanikisha jambo hili ni vyema sasa wananchi wa Nyasa watambue kuwa wilaya yao  ni muhimu kuboresha masuala ya uwekezaji, hivyo wananchi na viongozi wanalojukumu kubwa la kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya shughuli hii ili kuweza kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi”, alisema.

Aliongeza kuwa binadamu na shughuli zao, kila siku wamekuwa wakiongezeka lakini mazingira yaliyopo duniani hayawezi kuongezeka hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa binadamu kutunza rasilimali zilizopo ili zisiweze kuharibiwa kwa faida ya sasa na baadaye.

Kwa mujibu wa Dkt. Mahenge alieleza kuwa madhara ya uharibifu wa mazingira hayo ni pamoja na kukosekana kwa mvua ambazo binadamu hutegemea kwa kuendesha maisha yake ikiwemo shughuli za kilimo ili aweze kujipatia mazao ya chakula na biashara.


Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa amewataka wananchi wilayani humo kuongeza pia kasi ya upandaji miti kwenye maeneo yao ambayo ni rafiki ya mazingira katika utunzaji wa maji ardhini.

No comments: