Tuesday, June 13, 2017

ACACIA BADO KWA FUKUTA WAKANA RIPOTI YA PILI ILIYOCHUNGUZA MCHANGA WA MADINI

KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Acacia, imezikataa taarifa zote zilizotolewa katika ripoti ya Kamati ya pili iliyochunguza Makontena 277 ya mchanga wa madini yaliyozuiwa.

Acacia wamesema hayo ikiwa ni siku moja tu, baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli kupokea ripoti ya Kamati ya pili ya Wanasheria na Wachumi waliochunguza sakata hilo la mchanga wa madini.


Pia kampuni hiyo imetaka uchunguzi huru wa ripoti ya Kamati ya kwanza na ya pili zilizoundwa na Rais Magufuli kuchunguza mchanga huo.

“Migodi yetu inafanya kazi kihalali kwa kufuata sheria za Tanzania, hata usafirishaji wa mchanga huu unafanywa kwa kufuata sheria na kupata kibali cha usafirishaji,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa zuio la kusafirishwa mchanga huo haliiathiri Acacia pekee bali hata maisha ya maelfu ya Watanzania zaidi ya 36,200.


“Kampuni hii imekuwa ikiwekeza katika elimu, miundombinu na miradi ya afya na hivi vyote vitaathirika wakati zuio hili likiendelea”, imesema.

No comments: