Thursday, February 28, 2013

POLISI RUVUMA YAFANIKIWA KUNASA SILAHA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limefanikiwa kuzima tukio la ujambazi ambalo lilikuwa likifanywa katika mji wa Tunduru mkoni humo,  kwa kutumia bunduki ya kivita aina ya SMG.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Deusdedit Nsemeki alisema kuwa taarifa za kukamatwa kwa bunduki hiyo yenye namba 5637002531 zilifanikiwa baada ya jeshi hilo kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Alieleza kuwa bunduki hiyo bado haijajulikana inatoka nchi gani, na kwamba imepatikana baada ya polisi kupata taarifa za kiintelijensia, juu ya kuwepo mpango wa kufanyika tukio la ujambazi wilayani Tunduru.


Alisema kufuatia taarifa hizo pia jeshi la polisi lilifanikiwa kumnasa mtuhumiwa mmoja, aliyefahamika kwa jina la Jafar Hussein Abdalah na kwamba hadi sasa yupo mikononi mwa polisi na sheria zitafuata mkondo wake.

Kamanda Nsemeki alifafanua kuwa shughuli ya bunduki hiyo iliyokamatwa aina ya SMG ilikutwa ikiwa imefichwa katika kijiji cha Muungano mashambani.
Bunduki hiyo ya hatari ya tatu kukamatwa na polisi mkoani Ruvuma, katika kipindi kisichozidi miezi sita iliyopita, tangu kamanda huyo alipotangaza kutoa zawadi kwa mwananchi yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa bunduki zinazomilikiwa kinyume cha sheria.

“Hii ni bunduki ya tatu kukamatwa na polisi tangu mwezi Septemba mwaka jana kwa bunduki za aina hii, alisema Kamanda Nsemeki na kuongeza kuwa idadi hiyo haihusishi bunduki nyingine ndogo ndogo aina ya Shortgun, Rifle pamoja na risasi zake.

Alisema mafanikio hayo yanatokana na utekelezaji wa mpango wa polisi kwa kushirikiana na wananchi, kukamata silaha zote zinazomilikiwa kinyume cha sheria.         

No comments: