Saturday, February 9, 2013

MWENYEKITI JELA KWA KUTISHIA KUMUUA DIWANI


Na Steven Augstino,
Tunduru.

MWENTEKITI wa kata ya Nakapanya kwa tiketi ya Chama cha wananchi(UF)  Hassan Daimu Sinda, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi 16 jela baada ya kupatikana ha hatia ya uchochezi na kosa la kutishia.


Hukumu hiyo ilitolewa na mahakama  ya mwanzo Mlingoti mjini Tunduru baada ya kumtia hatiani katika makosa hayo ya kutishia kumuua  Diwani wa kata hiyo Mfaume Wadali, pamoja na kutoa tamko la kuwazuia wananchi kufanya kazi ya kujitolea yaliyofanyika Oktoba 28/2011.


Akitoa hukumu hiyo mbele ya mamia ya wananchi waliojitokeza kuisikiliza kesi hiyo ya jinai namba 21/2011 iliyohusu makosa ya kutishia kwa maneno kinyume na kifungu cha sheria namba 89 (2) (C) sura ya 16 kanuni ya adhabu na jinai namba 20/2011 ya kuwazuia wananchi kujitolea katika shughuli za maendeleo   kinyume cha kifungu
cha sheria namba 89 (2) (C)  sura ya 16 ya kanuni ya adhabu.




Akifafanu adhabu hizo Hakimu wa mahakama hiyo Abdalah Mponda alisema kuwa baada ya mahakama hiyo kupitia kanuni na vipengele vya sheria, ikiwemo kulinganisha na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo,  imemuona kuwa anayohatia hivyo inamuamuru  kutumikia adhabu ya miezi 4 jela ama kulipa faini ya shilingi 200,000 katika kosa la kutishia kuua kwa maneno.


Kuhusu upande wa kosa la jinai namba 20/2011 ya kushawishi wananchi wa kata hiyo kutoshiriki katika shughuli za kimaendeleo mahakama hiyo imeona kuwa ili iwefundisho kwa viongozi wengine ambao wanaona kuwa siasa ni sehemu ya kudidimiza maendeleo kwa wananchi wake mtuhumiwa huyo inafaa kutumikia adhabu ya miezi 12 jela bila kulipa faini.


Aidha mahakama hiyo pia imetoa nafasi ya mwezi mmoja kukata rufaa katika mahakama ya wilaya, endapo mtuhumiwa huyo atabaini kuwa hakutendewa haki katika hukumu hiyo.


Awali hakimu huyo alidai kuwa mshtakiwa huyo ambaye alifunguliwa mashauri hayo katika kituo cha polisi nakapanya 0ktoba 28/2011 yalifuatia matamshi aliyoyatoa mtuhumiwa huyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Chekechea katika shule ya msingi Nakapanya uliofanyika Oktoba 26/2011.


Akitoa utetezi wake kabla ya kutolewa kwa adhabu hizo  kiongozi huyo Hassan Sinda ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Nakapanya, aliomba mahakama hiyo impatie adhabu ndogo kwa vile yeye anasumbuliwa na magonjwa ya kifua kikuu, kisukari, moyo pamoja na kuwa tegemezi wa kusomesha watoto 4 na mama yake mzazi ambaye ni mzee sana.


Kufuatia hali hiyo pia Hassan Sinda akizungumza katika hali iliyoonesha kuwa adhabu hiyo ilimchanganya aliahidi kuangalia uwezekano wa kukata rufaa katika mahakama ya wilaya kama alivyo elekezwa kwa matumaini kuwa huenda huko ataonekana hana hatia.

No comments: