Saturday, February 9, 2013

WANANCHI WA TUNDURU HAWANA BARAZA LA NYUMBA NA ARDHI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI Wilayani Tunduru Ruvuma imeahidi kufuatilia, kusimamia na kuhakikisha kuwa Baraza la ardhi na nyumba linaanzishwa wilayani humo ili kuwapunguzia kero wananchi wake.

Kauli hiyo imetolewa na katika sherehe za maadhimisho ya siku ya sheria Tanzania, na mkuu wa wilaya ya Chande Nalicho wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya mahakama ya Wwilaya hiyo mjini Tunduru.

Kufuatia hali hiyo Nalicho akatumia nafasi hiyo kumtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, kuangalia uwezekano wa kuingiza suala la uanzishaji wa baraza hilo katika bajeti zake, ili angalau kuanzisha ujenzi wa majengo yatakayotumika katika shughuli hizo za kutafsiri sheria na kutoa haki kwa walengwa.


Aidha katika taarifa hiyo mkuu huyo wa wilaya, alisema kuwa kutokuwepo kwa baraza hilo tangu ianzishwe wilaya ya Tunduru, kumekuwa ni miongoni mwa vikwazo kwa wananchi wake pindi wanapokuwa na mahitaji ya kupata haki zao za kisheria, endapo mabaraza ya ardhi ya kata yatashindwa kuitatua migogoro hiyo.

Alisema kutokana na hali hiyo kumekuwa na tabaka la watu wa kupata huduma hiyo na kuwaacha wananchi wenye uwezo mdogo kifedha na wasiomudu kulipa nauli ya kati ya shilingi 20,000 na shilingi 5,000 kila wanapotakiwa kusafiri kufuata huduma hiyo muhimu, wamekuwa wakiacha haki zao zipotee kutokana na kukosa fedha za kuwawezesha kusafiri umbali wa kilometa 264 kutoka Tunduru hadi makao makuu ya mkoa wa Ruvuma mjini Songea ambako ndiko iliko mahakama hiyo.

Akizungumzia kukosekana kwa mahakama hiyo hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya Tunduru Ernest Mgongolo alidhibitisha kuwepo kwa kero hiyo, na kuongeza kuwa kukosekana kwa huduma hiyo kunawanyima haki ya msingi ya kisheria wanaokwazwa na madhila yatokanayo na kero mbalimbali za ardhi.

Kadhalika Mgongolo alikemea vikali tabai za wananchi kuchukua sheria mikononi kwa kuwapiga, kuwaua na kuwachoma moto watuhumiwa wa matukio mbalimbali  kuwa kwa kufanya hivyo wanakiuka uhuru wa binadamu na akawaasa kutoa ushirikiano kwa kuwakamata na kuwapeleka katika vyombo vya sheria na kuacha tabia ya kuchukua sheria mikononi.

No comments: