Wednesday, February 20, 2013

KAMPUNI YA GAME FRONTIERS YAFANIKIWA KUKAMATA PEMBE ZA NDOVU ZENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 192 WILAYANI NAMTUMBO MKOANI RUVUMA




Askari Wanyamapori wa pori la akiba Selou, wakiwa wameshika baadhi ya pembe za ndovu ambazo wamezikamata baada ya kuwakurupusha majangili waliokuwa nazo, wakitaka kutoroka nazo wilayani Namtumbo.





Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.

KAMPUNI ya Game Frontiers Tanzania(GFT) inayojishughulisha na uwindaji wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na kikosi cha askari wanyamapori katika pori la akiba la Selou, wamefanikiwa kukamata pembe za ndovu zenye thamani ya dola za kimarekani shilingi 120,000 sawa na fedha za kitanzania shilingi milioni 192.

Kaimu mkuu wa pori la akiba kanda ya kusini Magharibi Likuyuseka, Bernald Lijaji alisema tukio hilo lilitokea Februari 17 mwaka huu majira ya asubuhi, huko katika maeneo ya wazi jumuiya ya Mbarang'andu ambayo yamekaribiana na pori la akiba la Selou wilayani humo.
 

Lijaji alisema kwamba pembe zilizokamatwa zilikuwa 15 zenye  thamani ya fedha hizo, risasi tisa na bunduki mbili kati ya hizo moja ni aina ya Gobole na nyingine Raifo.


Aidha aliwaambia waandishi wa habari kuwa pembe hizo na bunduki zilizokamatwa hivi sasa vinashikiliwa katika ofisi ya Selou iliyopo wilayani Namtumbo na kwamba majangili waliokurupushwa na nyara hizo wametokomea kusikojulikana.

Alifafanua kuwa pembe hizo zilizokamatwa ni sawa na Tembo wa nane waliouawa, ambapo vitendo vya ujangili huo vimekuwa vikiwatesa kutokana na watu wasiokuwa waaminifu kuingia ndani ya pori na kuua wanyama bila kufuata taratibu na sheria za nchi.

Awali alieleza kuwa jitihada za kuwakurupusha majangili hao zinatokana na ushirikiano uliopo kati ya kampuni ya Game Frontiers(GFT), askari uhifadhi wa vijiji(VGS) na kikosi cha askari wanyama pori(Game reserve) cha Selou.

Mafanikio hayo yametokana na  kampuni ya GFT kuwezesha kutoa mafuta na gari ya doria, chakula, mawasiliano na kuwalipa posho askari ambao hushughulika katika kazi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mwakilishi wa kampuni hiyo inayojishughulisha na uwindaji katika pori la Mbarang'andu wilayani Namtumbo, Mohamed Mpapa alisema mafanikio hayo yanatokana na jitihada walizonazo na ushirikiano wa wananchi walio jirani na pori hilo.
 

Mpapa alitoa wito kwa jamii kuendelea kujenga ushirikiano, katika kuwafichua watu wanaohusika na vitendo vya ujangili kuua wanyama waliopo katika hifadhi na kutorosha nyara za serikali pasipo kufuata taratibu zilizowekwa na nchi.

No comments: