Saturday, February 9, 2013

BODI YA KOROSHO NA MWAROBAINI WA WALANGUZI WA ZAO HILO


Na Steven Augustino,
Tunduru.

BODI ya Korosho Tanzania imeahidi kutaifisha korosho zote ambazo hazitanunuliwa kupitia mfumo uliohalalishwa na serikali wa stakabadhi ghalani ikiwa ni juhudi ya kuendelea kulinda maslahi ya wakulima wa zao hilo.


Hayo yamebainishwa na bodi hiyo kupitia barua yake yenye kumbukumbu namba CBT/M/1/VOL  XXV/40 ya Januari 23 mwaka huu, ambayo imesambazwa katika wilaya zinazolima korosho na kuongeza kuwa tamko hilo limetolewa kufuatia kuwepo kwa mfumuko wa walanguzi wazao hilo ambapo wakulima huwanyonya kupitia vipimo haramu vya Kangomba.


Barua hiyo iliyosainiwa na Teofora Nyoni  kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa bodi hiyo, ilibainisha kuwa  ili kufanikisha zoezi hilo pia amewaomba wakuu wa wilaya, wakurugenzi, viongozi wa vyama vya ushirika vya wakulima kushirikiana na Jeshi la polisi kuwadhibiti na kuwakamata walanguzi hao.


Katika waraka huo ambao mwandishi wetu anayo nakala yake,
umewaelekeza viongozi hao kuutumia kuwashtaki wahalifu hao kupitia kifungu cha sheria namba 18 kanuni ya adhabu namba 69 ya mwaka 2009 inayoielekeza bodi hiyo kutaifisha korosho zote zinazonunuliwa na kusafirishwa isivyo halali na taratibu za nchi.



Alisema  pamoja na mamlaka hayo wanaoyopewa kuitaifisha korosho hizo kutoka kwa walanguzi hao,  pia bodi hiyo imepewa mamlaka ya kuziuza korosho hizo katika minada pamoja na kuwachukulia hatua za kuwashitaki ama kuwatoza faini isiyo pungua fedha za kitanzania shilingi milioni 3 walanguzi hao.

 
Akizungumzia tamko hilo Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho alisema barua na maelekezo yaliyotolewa na bodi hiyo ni msaada mkubwa kwa wakulima wa wilaya yake ya Tunduru na maeneo mengine kunakozalishwa zao hilo, ambao kwa kiasi kikubwa wamejeruhiwa na tabia mbaya za walanguzi hao.


Nalicho alieleza kwamba baada ya kupokea maelekezo hayo tayari ofisi yake imeandika barua  inayokazia maelekezo ya kuwadhibiti walanguzi hao, na kuisambaza kwa maafisa tarafa wilayani humo, watendaji kata na vijiji kuongeza juhudi za kuwadhibiti walanguzi hao na kwamba kiongozi atakayelegalega katika shughuli hiyo sheria itafuata mkondo wake.


No comments: