Saturday, February 2, 2013

MGODI WA MAKAA YA MAWE MBINGA WAZUA MALALAMIKO

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

WAKATI serikali ikiendelea kumaliza mgogoro wa kupinga kusafirishwa kwa gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, hali hiyo imehamia hapa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambapo juzi kundi la wakazi wa kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani humo, nalo lilikuja juu na kutaka kuandamana kwa muda wa masaa kadhaa kupinga kusafirishwa kwa makaa ya  mawe ambayo yanachimbwa kijijini humo.

Lengo la kutaka kufanya hivyo lilitokana na wakazi hao kudai nyongeza ya fidia zao katika eneo ambalo walihamishwa, kwa ajili ya kupisha kazi ya uchimbaji wa makaa hayo na kupinga juu ya uchafuzi wa maji katika mto Nyamabeva ambao unafanywa na wachimbaji wa madini hayo.

Maji ya mto huo yamekuwa yakitumika na wananchi hao kwa shughuli mbalimbali majumbani mwao, lakini hivi sasa wanashindwa kuyatumia kutokana na wachimbaji wa makaa hayo kutiririsha maji yenye mkaa wa mawe kuelekea kwenye mto huo, na kusababisha baadhi ya viumbe kama vile samaki kupoteza maisha ambapo serikali ya wilaya ya Mbinga baada ya kupata taarifa hizo, ilichukua jukumu la kwenda huko na kuamuru wachimbaji hao kuzuia maji hayo yasielekezwe katika mto huo.


Aidha kundi hilo lilikuwa likilalamika kwamba vumbi kali la mkaa wa mawe limekuwa likienea katika vijiji vilivyokuwa jirani na mgodi huo pale unaposafirishwa, ambapo walimtaka mwekezaji husika aangalie namna ya kulidhibiti ili wananchi wasiweze kuathirika afya zao.

Hali ilikuwa tete ambapo kamati ya ulinzi na usalama ngazi ya wilaya ikiongozwa na Mwenyekiti wake mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga, ililazimika kwenda huko kumaliza mgogoro huo ambao ulionekana kutaka kuhatarisha amani kati ya kampuni inayochimba mkaa huo, Tancoal Energy katika mgodi wa Ngaka, uliopo kijijini humo na wananchi kwa ujumla.

Ngaga na kamati yake baada ya kwenda huko Januari 29 mwaka huu, alifanya kikao na wananchi wa  kijiji cha Ntunduaro katika eneo la ofisi ya serikali ya kijiji hicho, na kuzungumza nao kwa kuwatuliza waache jazba wawe watulivu wakati serikali, inaendelea na mchakato wa kuyashughulikia madai yao.

Pamoja na hayo licha ya mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, kuwataka wananchi hao wafanye hivyo, bado wengine walionekana kulalamika kwamba kilio chao kimedumu kwa muda mrefu, wakidai kwamba wamechoshwa na ahadi ambazo hazizai matunda na utekelezaji wake unaonesha ukifanywa taratibu.

Vilevile Ofisa mtendaji wa kata ya Ruanda Matilda Nchimbi alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alisema mgogoro huo wa wakazi kijiji cha Ntunduaro, unatokana pia na kampuni hiyo ya Tancoal Energy kutokamilisha kwa muda mrefu kazi waliyoahidi ya ukarabati wa zahanati ya kijiji hicho, ujenzi wa visima vya maji na shule, jambo ambalo limekuwa likizua malalamiko miongoni mwa jamii.

Nchimbi alieleza kuwa tatizo lingine ni kwamba madai ya wakazi hao wanataka majibu yatolewe haraka juu ya uchafuzi wa maji ya mto Nyamabeva, ambao maji yake baada ya kuchafuliwa na mkaa wa mawe wataalamu wa mazingira kutoka wilayani humo walikwenda na kuchukua kiasi kidogo kwa ajili ya kuyafanyia uchunguzi wa kina, ili waweze kubaini madhara yake na kwamba hadi sasa ni muda mrefu umepita hakuna majibu yaliyotolewa.

Hata hivyo alipoulizwa msimamizi wa uchimbaji wa mkaa wa mawe katika mgodi huo wa Ngaka, aliyejitambulisha kwa jina moja la Hemedi alisema yeye akiwa kama mwakilishi wa kampuni, amepewa jukumu la kusimamia uchimbaji wa mkaa huo tu na hawezi kuzungumzia lolote juu ya malalamiko hayo.
 

No comments: