Tuesday, January 29, 2013

UPINZANI WAPATA PIGO TUNDURU

  Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma upande wa kulia Oddo Mwisho akipongezana na baadhi ya wazee wa Tunduru mara baada ya wanachama wa kambi ya upinzani kurudisha kadi zao na kuhamia CCM

 Na Steven Augustino,
Tunduru.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) katika Kata ya  Lingunga,  Mwenye Kwitanda akiwa na kundi la wanachama wake 300 wamehama chama hicho na kujiunga na  Chama  cha mapinduzi (CCM) ikiwa ni juhudi ya chama hicho kujiimarisha.

Hayo yalibainishwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo na
mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha mapinduzi(CCM) taifa wa wilaya
hiyo Ajiri Kalolo na kuongeza kuwa kati ya wanachama hao wanachama 200 wametoka CHADEMA, wanachama 60 wametoka CUF na wanachama 40 wametoka TLP.

Kalolo aliendelea kueleza kuwa wengi wa wanachama hao ni kundi la vijana ambao katika uchaguzi mkuu  wa mwaka 2010, walirubuniwa na kujiunga na  vyama hivyo kwa ahadi za kuyafikia maendeleo kwa urahisi lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea.


Alifafanua kuwa baada ya kubaini hali hiyo ambayo ilizua manunug’uniko mengi kutoka katika kundi hilo, wao kama wazee walilazimika kukaa na vijana hao na kuwaelekeza hali halisi ya janja za wanasiasa na kuwaeleza kuwa CCM ndicho chama chenye dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo.

Alisema katika harakati hizo wazee hao walitumia mifano mbalimbali ya utekelezaji wa miradi kupitia chama hicho, kuwa kinao ushahidi wa nini kimetekeleza kwa vitendo.

"Nawashukuru sana vijana, wazee na akina mama ambao mmeamua kurudi CCM chama ambacho kimeleta mabadiliko makubwa hapa kijijini Ligunga, msifanye tena makosa ya kuvichagua vyama vya upinzani kutuongoza, kwani havina sera hata moja inayoweza kutekelezeka kwenu", alisisitiza Kalolo.

Aidha aliwataka wakereketwa, wanachama wa chama hicho na wananchi kwa
ujumla kuachana na malumbano yasiyokuwa na maana, badala yake watumie muda wao mwingi kujiletea maendeleo ili kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza katika mkutano huo ulioandaliwa na mjumbe huyo wa NEC aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA katani humo Mwenye Kwitanda alisema
kimsingi, wanachama 200 wa chama hicho ambao wameamua kwa moyo wao
kurudi CCM, wamerejea nyumbani na kwamba aliwaomba wana CCM kuwapokea kwa mikono miwili.

Kwitanda aliendelea kufafanua kuwa wao waliamua kujiunga na chama hicho cha upinzani, baada ya kukatwa kwa jina la mgombea ambaye alikuwa kipenzi chao kwenye kura za maoni za mwaka 2010 ambapo mgombea ambaye jina lake lilirudishwa kugombea udiwani hakuwa chaguo lao.

"Labda tu niseme sisi tulihama CCM kutokana na mizengwe iliyojitokeza mara baada ya kukamilika kwa kura za maoni mwaka 2010, tuliyemchagua sisi alishinda kura hizo lakini wenzetu hawakurudisha jina lake pamoja na kuongoza, ndipo tukamshawishi agombee kupitia CHADEMA na kweli alishinda", alisema.

Alikitaka chama cha mapinduzi kuzingatia maamuzi ya wengi baada ya kura za maoni, ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima na kwamba wao wamerejea CCM kwa moyo wa dhati hivyo wanatarajia kupata ushirikiano wa hali ya juu, ili kukijenga chama upya katani humo.

            








No comments: