Friday, January 18, 2013

SOKO LA UHAKIKA ZAO LA KOROSHO TUNDURU LAZUA GUMZO, WAKULIMA WAIOMBA SERIKALI KURUHUSU KUUZA KWA WATU BINAFSI


Na Steven Augustino,
Tunduru.
 

WAKATI kukiwa na Sintofahamu juu ya upatikanaji wa soko la uhakika la kuuzia Korosho, wakulima wa zao hilo  wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali itoe kibali cha kuruhusu korosho zao kuuzwa kwa wafanyabiashara binafsi ili kuwaepusha na hasara wanayoendelea kuipata wakati  huu, ambapo wanasubiri malipo yao ya mwaka uliopita.

Kilio hicho kimepazwa kwa nyakati tofauti na wakulima hao, na kuungwa mkono na viongozi walioshiriki katika mkutano mkuu maalum wa chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru(TAMCU) kilichoketi kwenye ukumbi wa chama hicho, uliopo mjini hapa.


Wakifafanua taarifa hiyo wakulima hao walisema kuwa hali hiyo inatokana na  muda wa uvumilivu kupita na hata kuvuka kikomo, hivyo wameamua kuchukua maamuzi hayo ya kuitaka serikali, ichukue hatua haraka ili wasiendelee kupata hasara kama ilivyotokea katika msimu wa mwaka 2010/2011.


Walisema katika msimu huo zaidi ya tani 500 ya zao hilo hazikununuliwa hali ambayo iliwasababishia hasara na matatizo mengi, wakulima hao ambao kwa sasa hao hawataki kusikia tena neno la ushirika kwa kile walichodai kwamba  unawasababishia umasikini na kukubali kuuza mazao yao ikiwemo la korosho kwa walanguzi wanaonunua kwa bei ndogo kuliko kusubiri bei ya serikali ambayo haina uhakika.

Juma Kazembe, Dinani Mungwa na  Athuman Milanzi ni miongoni mwa wakulima waliochukua maamuzi hayo magumu ya kuvunja ukimya huo kwa serikali yao, na kueleza kuwa korosho za mwaka uliopita hazikununuliwa na Korosho za msimu huu hadi leo hii bado zipo mashambani lakini wakati huo serikali ikiwa imekaa kimya.

Walisema kuwa kufutia hali hiyo wao ndio wanaopaswa kulisemea hilo kwa Serikali yao, na wanaamini kuwa ombi lao litajibiwa kwani wanaoogopa kupata tena hasara.

Walisema mateso waliyoyapata katika msimu uliopita wa mwaka 2011/2012 ambao ulikuwa msimu wa mateso makubwa kwao, na hadi sasa baadhi yao kulazimika kuzikimbia nyumba zao kufuatia madeni makubwa wanayodaiwa katika taasisi za kifedha.

"Kuna wenzetu hivi sasa tunavyoongea na wewe hapa Tunduru hawapo tangu mwaka jana, na inasadikiwa kuwa wamekimbilia nchi Jirani ya Msumbiji kwa ajili ya kukimbia madeni ambayo tulikopa pesa kwa ajili ya kununulia pembejeo zilizotumika kupulizia Korosho msimu uliopita, kutoka benki kwa mategemeo tutalipa baada ya kuuza korosho zetu”, alisema Milanzi.

Nao wakulima wa kijiji cha Kitanda wilayani humo Said Masuud, Hashim Mpunga na  Brashi Mgoa katika malalamiko yao waliiomba serikali kuwalipa madeni yao mauzo ya korosho za mwaka jana, baada ya kujidhamini kwa chama cha ushirika wilayani humo(TAMCU) kupitia vyama vikuu vya ushirika(AMCOS) zichukue korosho zao kwa makubaliano kuwa watalipwa stahiki zao mara fedha hizo zitakapopatikana lakini hadi sasa wanaendelea kuteseka.

Walisema kutokana na hali hiyo kuwa kwa sasa wameshindwa kuendelea na shughuli za kilimo, kwani hawana fedha za kununulia pembejeo na hata katika mabenki ambayo ndiyo yalikuwa mkombozi wao, wanashindwa kwenda kukopa tena kutokana na kudaiwa kiasi kikubwa cha fedha na baadhi ya wenzao kutafutwa kwa kushindwa kurejesha mikopo yao.

Akizungumzia hali ya mkanganyiko huo Meneja wa chama kikuu cha ushirika cha wakulima wa Tunduru(TAMCU) Imani Kalembo alidai kuwa hali hiyo inatokana na chama hicho kukosa sifa za Kukopesheka baada ya kushindwa kurejesha deni la zaidi ya shilingi Bilioni.2.8 kati ya fedha zilizokopwa msimu uliopita.

Alisema ushirika huo ulishindwa kulipa deni hilo kufutia ubabaishaji wa wanunuzi wakubwa ambao walitelemsha bei kwa kiasi kikubwa, na kukifanya chama hicho kuuza korosho zao kwa bei ya shilingi 850 kwa kilo moja kutoka shilingi 1200 walizonunulia kutoka kwa wakulima na kusababisha kukumbwa na hasara.

No comments: