Tuesday, January 8, 2013

AUAWA NA MWILI WAKE KUTUPWA MASHAMBANI KUTOKANA NA UGOMVI WA KIMAPENZI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Tinginya tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru, Ruvuma amekutwa mwili wake ukiwa umetupwa katika mashamba ya kijiji hicho, baada ya kuuawa kikatili na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.

Marehemu ametambuliwa kwa jina la Abdallah Kingunge(35) ambapo kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walisema, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Januari 4 mwaka huu.

Walifafanua  kuwa mkasa huo umewasikitisha wengi na kuleta gumzo katika kijiji hicho na kutajwa kuwa huu ni mwanzo mbaya kwao kwa mwaka huu ni sawa na kutia nuksi kwa wanakijiji wa Tinginya ambao daima huishi kwa amani na upendo.


Kijana huyo inadaiwa amekutwa na mauti kutokana na kifo chake kuhusishwa na ugomvi wa kimapenzi.

Waliendelea kufafanua kuwa mkasa wenyewe ulianza baada ya marehemu Abdallah, kukutwa akijistarehesha kwa kinywaji cha pombe ya jadi nyumbani kwa mwanakijiji mwenzake aliyefahamika kwa jina la Anusa said ambaye ni muuzaji wa Pombe hizo.

Walisema akiwa mahali hapo ndipo sokomoko likazuka kwani tayari marehemu  alikuwa akituhumiwa muda mrefu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke wa Anusa Said aitwaye  Mwanahamis Said.

Walisema uwepo wake mahali hapo ndiko kuliko unganishwa na tukio hilo baada ya taarifa za awali za uchunguzi, kuonesha kuwa tayari kulikuwa na kutafutana na hata kurushiana maneno kati ya Anusa na mtuhumiwa wake wa ugoni marahemu Kingunge.

Taarifa zilizotolewa na mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marahemu huyo, Dkt. Jeshi Daraja zinasema kuwa chanzo cha kifo hicho ni kutokwa na damu nyingi kuliko sababishwa na kuchomwa kisu Tumboni, shingoni na kifuani.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Deusdedith Nsemeki alisema mwili wa Abdallah umekutwa alfajiri ukiwa umetupwa mashambani huku ukiwa na majeraha ya kupigwa na vitu vizito na vitu vyenye ncha kali.

Kamanda huyo wa polisi alieleza kuwa tayari Polisi inawashikilia Anusa na mkewe Mwanahamis kwa tuhuma za mauaji hayo hadi uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

No comments: