Friday, January 4, 2013

TANESCO MBINGA MASWALI MENGI KULIKO MAJIBU

Kassian Nyandindi



















Na Kassian Nyandindi,                                         Uchambuzi.

TATIZO la upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mji wa Mbinga, hivi sasa imekuwa ni kero kiasi ambacho wakazi wa mji huo wameanza kulalamikia hali hiyo.

Binafsi nimelichunguza tatizo hili na kubaini  TANESCO kuanzia ngazi ya wilaya hadi huko juu, ni muhimu kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo ili isiweze kuendelea na kuleta malalamiko yasiyo ya lazima miongoni mwa jamii.

Ukosefu wa umeme wa uhakika katika mji huu wa Mbinga unatokana na Transfoma yenye ukubwa wa KVA 100 – 11KV kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo kwa sababu ya kubebeshwa mzigo mkubwa nje ya uwezo wake.

Transfoma hiyo ndio kiini kikuu ambacho hutegemewa kusambaza nishati hiyo muhimu katika maeneo ya viwanda, mashine za kukobolea nafaka na maeneo mengine ya nyumba za kuishi watu.


Ninachoweza kuuliza hapa ni kwamba TANESCO Mbinga mlikuwa mkifanya nini siku zote hizi hadi Transfoma hii inazidiwa katika kufanya kazi yake, ukizingatia kwamba wateja Mbinga sasa wanaongezeka kila kukicha.

Huu ni uzembe, kwa sababu binafsi natambua mlikuwa mkijua kwamba kadiri wateja mnavyozidi kuwaunganishia “Service line” walikuwa wakiongezeka, sasa mlikuwa wapi kutafuta Transfoma nyingine ya akiba ili kunusuru hali hii isiweze kutokea?

Katika maeneo ya viwanda na mashine ya kukobolea nafaka hapa Mbinga mjini, tunakosa huduma husika kutoka katika maeneo hayo na kutufanya shughuli zetu za kimaendeleo zishindwe kutekelezwa ipasavyo, yatupasa tuelekeze lawama zetu kwenu.

Lawama hizi apelekewe nani kama sio ninyi, ambao mmeshika hatamu ya kuongoza na kusimamia shirika hilo la ugavi wa umeme hapa Mbinga.

Hivi sasa umeme unaosambazwa katika mji huu sio wa uhakika hivyo, ofisi ya TANESCO ifanye  mawasiliano na ofisi husika ili tuweze kuletewa transfoma nyingine haraka, kwa ajili ya kuongeza nguvu ya usambazaji wa nishati hiyo.

Nakumbuka majira ya saa nane mchana Desemba 31 mwaka jana, ndipo tatizo hili lilianza kujitokeza baada ya wateja wenu kuwapigia simu kuwa transfoma iliyopo eneo la ofisi za idara ya ujenzi inatoa moshi na mlipoichunguza mlibaini kuwa imezidiwa, sasa tunahitaji utekelezaji wa haraka ili tuondokane na kero hii.

Hata hivyo Meneja wa shirika hilo la ugavi wa umeme hapa Mbinga Kanut Punguti, nimemnukuu akisema kasi ya upatikanaji wa transfoma nyingine itategemea na mchakato utakaofanywa na uongozi wa shirika hilo ngazi ya mkoa.

Nasema kauli hii inakatisha tamaa, na inaonesha upatikanaji wa chombo hiki utachelewa na wala tusitegemee kupata haraka, je tutafika kweli?

Ni vyema sasa uongozi wa Taifa makao makuu ya TANESCO, waingilie kati suala hili, ili wanambinga tuweze kupata umeme wa uhakika kama ilivyokuwa awali, hatuhitaji kupewa kauli ambazo utekelezaji wake unaonesha kwenda polepole.


No comments: