Friday, January 18, 2013

WANANCHI WAHOFIA KUKOSA MAWASILIANO KUTOKANA NA BARABARA YA KUTOKA TUNDURU KWENDA SONGEA KUWA KATIKA HALI MBAYA





Hii ndiyo adha iliyopo barabara ya kutoka Tunduru kwenda Songea mjini. Serikali yaombwa kuingilia kati kwa kuchukua hatua za haraka katika kunusuru hali hii.(Picha na Steven Augustino)






 
Na Steven Augustino,
Tunduru.


WANANCHI wanaosafiri kupitia barabara ya Tunduru, kuelekea makao makuu ya mkoa wa Ruvuma, mjini Songea wamehofia kukosa mawasiliano na wenzao kufuatia barabara hiyo kuharibika vibaya, hasa kipindi hiki cha masika ambacho mvua nyingi zinaendelea kunyesha.

Baadhi ya abiria hao wakizungumza kwa nyakati tofauti ambao walifahamika kwa majina ya Mwanahawa Abdalah, Charles Haule na Asha Mohamed  walisema, barabara hiyo  ambayo kwa sasa inaelekea kuwa katika hali mbaya huenda ikajifunga kabisa na kusababisha magari ya abiria kushindwa kupita.  

Walisema hali hiyo imekuwa ni kero kubwa kwao na hivyo kusababisha nauli kupanda mara dufu  kutoka shilingi 15,000  hadi na wakati mwingine kufikia shilingi 35,000  jambo ambalo ni usumbufu kwa wananchi na jamii kwa ujumla.  


"Hii barabara kwa sasa haiwezekani tena kupitika tangu hawa Wahindi waliopewa jukumu la kuijenga waiharibu, kumekuwa na usumbufu mkubwa na kulazimika baadhi ya magari kushindwa kutoa huduma”, alisema Ally Seleman.

Aidha kufuatia kukatika kwa mawasiliano hayo ya barabara kati ya Songea na Tunduru pia hali ya maisha kwa wakazi wa Tunduru yamezidi kuwa magumu, ukizingatia kwamba wamekuwa wakitegemea kupata huduma muhimu au zaina mbalimbali kama vile nguo, mafuta na hata baadhi ya vyakula kutoka mjini songea.
 
Awali barabara hiyo ambayo serikali iliimpatia mkandarasi wa kampuni ya “Progresive” kutoka India ili aitengeneze kwa kiwango cha lami, hali imekuwa tete baada ya mkandarasi huyo kushindwa kufanya kazi hiyo na serikali kulazimika kuchukua hatua ya kumnyang’anya na sasa  imechimbika na kuwepo mashimo makubwa, yenye kujaa maji hivyo kuna kila sababu ya kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo ikiwemo kumtafuta mkandarasi mwingine, ambaye ataweza kujenga barabara hiyo kwa kiwango kinachokubalika.

Akizungumzia hali hiyo mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho aliyetembelea kuona uharibifu huo wa mvua ambao umefanywa katika barabara hiyo alisema, kwa sasa wakazi wa wilaya yake hawana namna, kwani barabara hiyo haipitiki na kwamba uharibifu huo unachangia ugumu wa maisha ya wakazi hao.

Nalicho aliongeza kuwa hivi sasa wanachosubiri ni huruma ya serikali kupitia wakala wa barabara (TANROAD) mkoani Ruvuma, kufanya marekebisho ya haraka  sehemu zilizoharibika hasa katika kijijicha Chacha wilayani Namtumbo, ambako kuna magari   mengi yamekwama na baadhi yake yakiwa na bidhaa mbalimbali zikiwemo shehena ya mbolea kwa ajili ya wakulima kukuzia mazao mashambani.

"Barabara ya namna hii sijawahi kuiona katika maisha yangu, hakuna hata sehemu ya kupita maeneo yote ni mashimo, nawaomba sana wenzetu wa Tanroad kurekebisha maeneo mabovu kabla mvua haziendelea kunyesha kwa wingi", alisema mkuu huyo wa wilaya ya Tunduru.

Mkuu huyo wa wilaya  amewataka wananchi kuwa na subira wakati huu mgumu, ambapo serikali inaangalia namna ya kuifanyia matengenezo ya haraka barabara hiyo, huku ikisubiri kumpata mkandarasi atakaye endelea na ujenzi kwa kiwango cha lami ili waweze kuondokana na adha hii iliyopo sasa.


No comments: