Tuesday, February 19, 2013

MAUAJI Z'BAR: PADRI MWINGINE APIGWA RISASI TATU KICHWANI, TIMU YA MAKACHERO YATUMWA, JK AOMBELEZA, WATATU MBARONI, WAUMINI WAANGUA KILIO

PADRI wa Kanisa Katoliki la Minara Miwili, lililopo Mji Mkongwe, Zanzibar, Evaristus Mushi, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi tatu kichwani na watu wasiofahamika jana asubuhi.
 
Tukio la mauaji hayo limeibua simanzi kubwa kwa waumini wa kanisa hilo ambao jana walikusanyika kanisani hapo baadhi yao wakilia, kulaani mauaji ya kinyama aliyofanyiwa kiongozi huyo.

Baadhi ya waumini hao, walihoji utekelezwaji wa tamko la Serikali baada ya Padri wa kanisa hilo, Parokia ya Mpendaye mjini Zanzibar, Ambrose Mkenda, kujeruhiwa kwa risasi Desemba 24,2012 na watu wasiofahamika akiwa nje ya nyumba yake.

Baada ya tukio hilo, Desemba 28,2012 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ilitoa tamko la kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya mfululizo wa matukio ya kushambuliwa viongozi wa
dini ili kubaini kama ni hujuma zinazofanywa na baadhi  ya watu wanaotaka kuifanya Zanzibar isitawalike.



Tamko hilo lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohammed Aboud Mohamed, baada ya kumjulia hali Padri Mkenda, aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI).

Taarifa zilizolifikia gazeti hili, zinasema Padri Mushi alivamiwa  na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki aina ya Vespa, baada ya kushuka katika gari lake ili kwenye Kanisa la Betras.

Baada ya tukio hilo, Padri Mushi alikimbizwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja lakini baadaye alifariki dunia.

Rais Kikwete

Kutokana na tukio hilo, Rais Jakaya Kikwete, ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya nguvu zake zote na kuhakikisha linafanya uchunguzi wa kina na haraka ili kuwabaini wahusika waliofanya tukio hilo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema Rais Kikwete amelitaja jeshi hilo kushirikiana na vyombo vingine vya usalama nchini
na mashirika ya upepelezi kutoka nchi rafiki ili kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.

“Nataka umma ufahamu ukweli ili kama kuna jambo lolote zaidi liweze kushughulikiwa na kukata mzizi wa fitina, nimepokea taarifa za mauaji haya kwa mshtuko na masikitiko makubwa.

“Naomba nitumie fursa hii kutuma salamu za rambirambi kwa Baba Askofu, Augustino Shayo wa Jimbo Katoliki, Zanzibar na waumini wote wa Parokia ya Minara Miwili kwa msiba mkubwa ambao umewakuta,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza;

“Napenda kuwahakikishia kuwa, tupo pamoja katika kuomboleza kifo cha Mpendwa wetu Padri Mushi...msiba huu ni wetu sote,” alisema Rais Kikwete.

IGP Mwema azungumza

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, Alisema Makao Makuu ya jeshi hilo Dar es Salaam, limepeleka timu ya wataalamu waliobobea katika masuala ya upelelezi na opereshini mjini Zanzibar.

Alisema wataalamu hao watashirikiana na wenzao waliopo Zanzibar ili kufanya uchunguzi wa kina juu ya mauaji ya Padri Mushi pamoja na kutumia fursa hiyo kulaani kitendo hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari, IGP Mwema alisema hadi jana mchana, jeshi hilo lilikuwa linawashikilia watu watatu ambapo timu ya watalamu hao, inaongozwa na Makamishna watatu.

“Naibu Kamishna wa Polisi Peter Kivuyo, atahusika kukusanya taarifa za matukio, Naibu Kamishna Samson Kasela ambaye atahusika na masuala ya upelelezi wakati Mkuu wa Operesheni wa jeshi hilo, Simon Sirro atahusika na operesheni.

“Nawaomba wananchi wote mtusaidie kutoa taarifa juu ya watu wanaofadhili makundi yanayovuruga amani ya nchi, kuchochea na kushawishi...huu ndio mkakati mpya wa jeshi letu ambao umeazimiwa mkoani Dodoma,” alisema IGP Mwema.

Aliongeza kuwa, hivi sasa jeshi hilo limeimarisha doria katika maeneo yote nchini, kufuatilia mienendo ya watu wanaochochea, kufadhiri, kuhamasisha na kushiriki vitendo vya uhalifu, vurugu na fujo hivyo aliwataka wananchi kuwa watulivu.

IGP Mwema aliwataka wananchi wote wenye taarifa ambazo zitasaidia kukamatwa wahalifu hao, wapige namba 0754 785557, 0782 417247 au kuwapigia makamanda wa vikosi ili kuhakikisha amani, usalama na utulivu vinadumishwa nchini.

Waziri Mkuu Pinda


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, jana alikutana na viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo mkoani Geita na kuwataka watumie mkutano huo kwa manufaa ya Taifa  ili kuleta amani na utulivu nchini.

Alisema tukio la kuuawa Padri Mushi huko Zanzibar, limemsikitisha sana na kuongeza kuwa, huenda likawa na uhusiano na vurugu zilizotokea mkoano Geita, kati ya Waislamu na Wakristo.

Mashuhuda wa tukio

Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo, walisema Padri Mushi huwa na kawaida ya kwenda kusalisha katika Kanisa la Mtoni na alipofika kanisani hapo wakati akipaki gari lake, ghafla walitokea watu wawili, kumpiga risasi na kukimbia kusikojulikana.

“Hili kanisa lipo njiani kabisa, wakati tukipita tulisikia milio ya risasi...tulisogelea eneo husika la tukio na kukuta Padri Mushi akitokwa na damu nyingi kichwani,” walisema mashuhuda hao.

Waumini wake

Wakizungumza kwa masikitiko makubwa, waumini wa kanisa hilo walisikitishwa na mauaji hayo na kuiiomba Serikali ifanye uchunguzi wa kina ili wahusika waweze kukamatwa.

“Tumetoka nyumbani tukiwa na matumaini makubwa ya kufanya ibada na Padri Mushi lakini tulipofika kanisani tukapata taarifa za kusikitisha...mbona Zanzibar haina amani tena maana tumeingiwa hofu ya kuendelea kuishi hapa visiwani,” walisema.

Mwili wa Padri Mushi umehifadhiwa katika mochali ya Hospitali Kuu Mnazi Mmoja. Kiongozi mwingine wa dini aliyefanyiwa unyama hivi karibuni ni Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Shekhe Fadhil Soraga, aliyemwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.

Matukio ya viongozi wa dini kushambuliwa, yametanguliwa na uchomwa moto baa 12 na makanisa 25, katika maeneo tofauti visiwani Zanzibar.(Source, Majira Newspaper)

No comments: