Thursday, January 8, 2015

SERIKALI KUJENGA RELI KUTOKA MTWARA HADI MBAMBA BAY, WALIOVAMIA MAENEO YA UWANJA WA NDEGE SONGEA NA KUJENGA MAKAZI WATAKIWA KUONDOKA

Dokta Harrison Mwakyembe.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WAZIRI wa uchukuzi Dokta Harrison Mwakyembe amesema, serikali nchini imedhamiria kujenga reli kuanzia Mtwara hadi Mbamba Bay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, jambo ambalo litarahisisha kazi ya ubebaji wa mizigo mizito ya makaa ya mawe na chuma kutoka Liganga wilayani Ludewa mkoa wa Njombe.

Akizungumza na Wadau wa usafirishaji jana katika ukumbi wa Ikulu ndogo mjini hapa, Dokta Mwakyembe alisema ujenzi wa reli hiyo unatarajiwa kuanza mapema mwakani na kwamba utakamilika mwaka 2018.

Alisema kujengwa kwa reli hiyo kutasaidia barabara za lami zilizopo na zinazoendelea kujengwa katika mikoa ya kusini, kutoharibika mapema kutokana na kupitisha magari yanayobeba mizigo ya makaa ya mawe na chuma na kuzifanya zidumu kwa muda mrefu.


“Kujengwa kwa reli hii kutoka Mtwara hadi Mbamba bay kutakuwa na vituo saba na ujenzi huu utagharimu shilingi bilioni 3.5 hadi kukamilika kwake, lakini kukamilika huko kutasaidia sana kuzifanya barabara zetu zidumu kwa muda mrefu kutokana na ukweli kwamba, ile mizigo ya makaa ya mawe na chuma toka Liganga yatasafirishwa kwa njia ya reli”, alisema Dokta Mwakyembe.

Kuhusu ujenzi wa meli mpya itakayosaidia kurahisisha usafirishaji wa abiria katika ziwa Nyasa, alisema mkataba wa ujenzi unatarajiwa kusainiwa mwezi huu na kwamba baada ya hapo kazi ya ujenzi wa meli hiyo utaanza mara moja, ambapo kukamilika kwake kutasaidia pia kuwaondolea adha ya usafiri wananchi.

Pamoja na kujengwa kwa meli hiyo, mpango uliopo ni kuboresha bandari ya Itungi na Ndumbi ambapo mpaka sasa mamlaka ya bandari imetenga kiasi cha shilingi milioni 500, kwa ajili ya ujenzi wa ghati katika bandari ya Ndumbi.

Katika hatua nyingine Dokta Mwakyembe alipozungumza na wafanyakazi wa kiwanja cha ndege mjini Songea, alisema serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kuwa miundombinu ya viwanja vya ndege nchini, inaendelea kuboreshwa na kuweza kutoa huduma za kuridhisha kwa wananchi.

Alisema Mamlaka ya viwanja vya ndege ilifanya mazungumzo na benki ya dunia ili kutumia fedha zilizosalia katika mkopo uliowezesha ukarabati na upanuzi wa viwanja vya Kigoma, Tabora na Bukoba, kutekeleza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika viwanja kumi na moja ambavyo ni Songea, Iringa, Lake Manyara, Musoma, Tanga, Kilwa Masoko, Lindi, Moshi, Njombe, Singida na ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege mkoani Simiyu.

“Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015 serikali kupitia mamlaka ya viwanja vya ndege, tumetenga shilingi milioni 660 za kitanzania toka fedha za ndani na shilingi milioni 3,200 fedha za kigeni kutoka benki ya dunia, kwa ajili ya mradi wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa viwanja kumi na moja”, alisema.

Hata hivyo Waziri huyo aliwataka wananchi waliovamia eneo la uwanja wa ndege Songea na kujenga makazi ya kudumu, waondoke mara moja kwenye maeneo hayo na kwamba hakuna fidia yoyote itakayotolewa kutokana na hilo.


No comments: