Thursday, January 1, 2015

WAKULIMA WALIA NA MVUA, MAZAO YAO YAKAUKA SHAMBANI

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

KUCHELEWA kunyesha kwa mvua katika maeneo mbalimbali mkoani Ruvuma, kumesababisha wakulima kupatwa na wasiwasi juu ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, katika msimu huu wa kilimo hasa ikizingatiwa kuwa misimu iliyopita mvua ilikuwa ikianza kunyesha mkoani humo katika mwezi Novemba tofauti na ilivyo sasa.

Katika maelezo yao kwa waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wakulima wa wilaya za Namtumbo na Songea mkoani humo walisema, hali hiyo ya mvua kuchelewa kunyesha imeshaanza kuwatia hofu kubwa kwani tayari walishafanya maandalizi yote ya kilimo, ikiwemo kupanda mazao mashambani lakini hadi sasa mvua imekuwa ikinyesha kwa kusuasua.

Walisema hadi sasa mazao waliyopanda yameanza kuota lakini yanakauka kutokana na kukosekana kwa mvua za kutosha na kwamba hata wadudu wamekuwa wakijitokeza na kushambulia mimea iliyoota. 


“Mwakani tuna wasiwasi sana juu ya hali ya chakula katika mkoa huu, kwani mvua ambazo tunazitegemea kuanza kunyesha mwanzoni mwa mwezi Novemba mvua zimekuwa zikinyesha kwa suasua,  na mazao yanakauka shambani kutokana na kukosa maji ya kutosha”, walisema.

Naye Damas Hyera mkulima wa kijiji cha Liganga wilaya ya Songea alisema, upungufu huu wa mvua ulioanza  kujionyesha sasa katika maeneo mbalimbali ni ishara tosha ya wananchi kujiwekea akiba ya chakula kwani inawezekana kukatokea baa  kubwa la njaa katika msimu huu wa 2015 – 2016 na kwamba ni vyema serikali ikaanza kuchukua hatua madhubuti ya kukabiliana na hali hiyo.

Naye Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akifafanua juu ya hali hiyo aliwataka wakulima wa mkoa huo kuzalisha mazao yanayostahimili ukame kama vile mhogo, na kwamba aliwaaagiza maafisa kilimo kuacha kukaa maofisini badala yake wapiti vijijini na kutoa elimu kwa wakulima kuhusiana na uzalishaji wa mazao hayo ambayo yanastahimili ukame.

Mwambungu aliongeza kuwa kila kaya inapaswa kujenga tabia ya kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha, kulingana idadi ya familia ili kuepuka uwezekano wa kupatwa na njaa jambo ambalo ni nadra kujitokeza katika mkoa huo.


No comments: