Thursday, January 8, 2015

WANUSURIKA KIFO BAADA YA KUPIGWA RISASI NA MAJAMBAZI



Na Gideon Mwakanosya,

Songea.


JESHI  la Polisi mkoani Ruvuma linawasaka watu wanne  wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao wanadaiwa kuwapiga risasi watu wawili, katika matukio tofauti likiwemo la mwanamke  ambaye ni mhudumu wa baa kujeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi mgongoni, kisha kunyanganywa simu ya  mkononi yenye thamani ya shilingi 35,000 na kutokomea nayo kusiko julikana.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema kuwa matukio yote mawili yametokea majira ya saa za usiku  huko katika maeneo ya Mabatini kata ya Misufini na Mfaranyaki mjini songea.

Kamanda Msikhela alisema kuwa  tukio la kwanza lilitokea  majira ya saa mbili usiku huko katika mtaa wa mabatini kwenye eneo la kando kando ya ukuta  wa msikiti wa , uliopo kata ya Misufini ambapo Fatuma Hamisi (29) ambaye ni mhudumu wa baa ya Olympic iliyopo mjini hapa, wakati akielekea kazini kwake ghafla alifuatwa na kijana  mmoja mwembamba aliyevalia kofia aina ya mzura ambaye hakufahamika kwa jina, na kumuamuru Fatuma asimame.


Alisema kuwa wakati Fatuma anamsimamisha, kijana huyo aliamua kutoa silaha ambayo baadaye alifyatua risasi moja hewani huku akimtaka amkabidhi simu aliyokuwa nayo mkoni lakini, msichana huyo aliendelea kugoma kumpatia simu kisha alimfyatulia risasi nyingine mgongoni na kumnyanganya simu aina ya ITEL yenye thamani ya shilingi 35,000.

Kwa sasa hivi Fatuma amelazwa katika hospitali ya mkoa Songea, kwa matibabu zaidi na hali yake bado ni mbaya kwani madaktari wanaendelea kumfanyia uchunguzi zaidi.

Kamanda Msikhela alieleza kuwa hivi sasa jeshi la polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa wa tukio hilo, ambalo limeleta hofu kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.

Alilitaja tukio lingine kuwa lilitokea January 8 mwaka huu majira ya saa tisa usiku kwenye maeneo ya mtaa wa gereji ya kisiwa kata ya Mfaranyaki Manispaa ya Songea, ambako  Mussa Mchopa (50) ambaye ni Meneja wa baa ya Sovi mjini humo akiwa amelala nyumbani kwake alivamiwa na  kundi la watu wanne wasiofahamika ambao kabla ya uvamizi huo walivunja mlango na kuingia ndani ya nyumba hiyo.

Watu hao wanaodaiwa kuwa  ni majambazi wakiwa ndani ya nyumba hiyo walimvamia Mchopa na wakati wa kurupushani hizo, Mchopa alipambana na watu hao huku tayari wakiwa wamemjeruhi kwa kumpiga risasi eneo la kichwani na baadaye walikimbia bila kuchukua kitu chochote.

Wakati wanakimbia  walidondosha bunduki aina ya CHINESE PISTOL yenye namba za usajili  2000911 ambayo ilikuwa na risasi saba, huku ganda moja la risasi limekutwa kwenye eneo la tukio na polisi inaendelea kufanya uchunguzi ili kuwapata watuhumiwa wa matukio yote mawili.

Alieleza majeruhi Mchopa ametibiwa  katika hospitali ya mkoa Songea na ameruhusiwa na hali yake inaendelea vizuri.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa Songea Dokta Benedict Ngaiza alisema kuwa usiku wa kuamkia jana, majeruhi wawili wamepokelewa ambao wanadaiwa kuwa walipigwa risasi katika matukio mawili tofauti ambapo alidai kuwa Fatuma ambaye amelazwa katika wodi  namba mbili ya majeruhi hali yake bado si nzuri, na uchunguzi unaendelea kufanywa kwani alipigwa risasi mgongoni ambako kuna jeraha kubwa na Mchopa aliletwa hospitalini hapo akiwa na jeraha kichwani ambalo inadaiwa alipigwa risasi na watu wasiofahamika lakini ameruhusiwa na hali yake inaendelea vizuri.

No comments: