Sunday, January 18, 2015

TUACHE KUCHEZEA AMANI YA TANZANIA, POLISI TUPATIENI UKWELI JUU YA PANYA ROAD

Padre Baptiste Mapunda.

Na Padre Baptiste Mapunda,

WATAALAMU siku zote wanasema mwanzo mbaya huashiria mwisho mbaya, hivyo basi kwa kauli hii mwaka huu 2015 Watanzania waishio Jijini Dar es Salaam  wameuanza vibaya kwa kutikiswa na kikundi cha “Panya Road.” 

Siku ya tarehe moja Januari ya kila mwaka duniani husherehekewa kama siku ya amani duniani, na amani hii tunayoitamka hapa ni ile inayotoka kwa Mungu na siyo ya bunduki wala mabomu.

Baba Mtakatifu kila mwaka huwa anatoa ujumbe wa amani kwa watu wote waliowakristo na wasiowakristo, mwaka huu ujumbe wake ulibeba kauli ya “sasa hakuna mtumwa” kwani sote ni kaka na dada. 

Nilivyomwelewa Baba Mtakatifu Francis anamaanisha kwamba utumwa wa aina yeyote ile ni alama ya kukosekana kwa amani moyoni, familia, jamii na dunia kwa ujumla wake. 

Duniani tumwa ni nyingi mathalani utumwa wa mawazo, wa kukosa uhuru, haki za binadamu, utumwa wa dhambi, wa kutawaliwa na hata ule wa umaskini. Watu wa jiji la Dar es Salaam mwaka huu walianza na utumwa wa kukosa amani ya kutembea kwa uhuru na furaha, kwa sababu ya  ujambazi, uhuni na uhalifu wa kikundi cha Panya Road.


Wakati  wananchi wengi wakilalamikia uhalifu  wa panya road na kuihoji serikali na jeshi la polisi lenye jukumu la kulinda amani ya  raia na mali zao, Polisi jijini Dar es salaam  kupitia Kamanda wao Suleiman Kova amekuwa akitoa majibu yanayokinzana. 

Mara ya kwanza alisema kwamba, hiki ni kikundi cha vijana wasiozidi kumi na tano hivi na wala hakina madhara kwa jamii.

Lakini baada ya siku chache kamanda huyo huyo, alisikika anaripoti kwamba kulikuwa na vijana zaidi ya 500 wakijihusisha na  kikundi hiki cha panya road. Na baadaye kidogo ripoti ilisema  sasa ni vijana zaidi ya elfu moja wamekamatwa katika uhalifu wa panya road.

Kwanza neno lenyewe “Panya Road” nimekuwa nikijiuliza maswali mengi maana yake ni nini, na msamiati huu  umetungwa na nani, maana yake ni nini katika jamii ya watanzania labda jeshi la polisi wangetupa asili ya neno hili, linatokana na nini na lina  ashiria nini?

Kitu cha kujiuliza neno panya, hawa ni viumbe wadogo tena wenye woga mkubwa je, wanawezaje kuwatisha wanadamu wakiwamo polisi wenye ujuzi na ukakamavu wa kushughulika na kulinda amani ya jamii?

Mbaya zaidi tumesikia pia jeshi la polisi likitoa tafsiri ya Panya road kwamba ni vijana wavuta bangi, wazurulaji, waosha magari, vibaka, wezi nakadhalika. 

Vijana wazururaji ni wazururaji, na wavuta bangi nao wanajulikana kwa uvutaji bangi, wezi wanaitwa wezi, waosha magari nao vile vile. Ifahamike kwamba siyo kila kijana mzurulaji au mwosha magari au mvuta  bangi ni mhalifu la hasha!

Polisi mtuambie panya road ni nani, na mbaya zaidi inaonekana wazi kwamba baada ya kushindwa kuwapata vijana panya road basi polisi waliamua kuwakamata vijana wa makundi yaliyotajwa hapo juu na kuwafanya ndiyo wawajibike na uhalifu wa panya road. Je hii ni sahihi kuunganisha vijana wote katika kundi la panya road?

Hii siyo sahihi, huku ni kutafuta majibu mepesi  kwa maswali magumu, huu ni uzugaji na uendelezaji wa sinema ambazo zimeendela kugonga mwamba kama ile ya mtekaji wa Dokta Ulimboka, ambaye alisemwa na kamanda Kova kwamba alikuwa ni Mkenya. Mimi naona kwamba Jeshi la polisi nchini linaendelea kuchezea amani ya Tanzania ambayo ni tunu kwa taifa letu, iliyotoka kwa mwenyezi Mungu.

Mara nyingi imetokea katika nchi za Afrika kwamba, chama tawala kinapokaribia kupokonywa madaraka kwa sababu ya kuchokwa na wananchi huwa kinaendekeza vikundi vya kihalifu  ambavyo baadaye vinaweza kutumiwa na watu wenye nia mbaya, kuharibu shughuli ya uchaguzi mkuu. 

Kule nchini Kenya kumekuwa na kikundi cha Mungiki, kikundi cha vijana walioanza kama kimzaha mzaha kama kilivyo kwa hawa panya road, wakakiiita kikundi cha vijana wahuni tu. Lakini baadaye kikundi hiki kilitumiwa na wanasiasa ili kudhuru na kuua wapinzani na wakosoaji wa chama tawala hasa enzi za KANU chini ya Rais Arap Moi.

Leo ninaposikia ubabaishaji wa jeshi la polisi juu ya kikundi hiki maarufu kama panya road, naanza kuwa na wasi wasi mkubwa juu ya utendaji wa jeshi letu la polisi hasa kuelekea uchaguzi mkuu. Hiki kikundi mimi nakiona ni kikundi cha wahuni, majambazi na wahalifu ambao huenda wamefadhiliwa na baadhi ya watu wenye pesa ili kuweza kuwatisha wananchi, kuwajeruhi na hata kuwaua  raia. Hayo nayasema na kuyaandika  kutokana na maono niliyoyadokeza wiki jana katika gazeti la Mwananchi pamoja na kusoma alama za nyakati.

Sote tunafahamu kwamba mwaka huu mwezi wa Aprili, tutakuwa na upigajikura wa maoni ya kuikubali au kuikataa katiba pendekezwa ya CCM. Mimi kama nilivyoandika awali kwamba kura yangu  itakuwa ni ya “hapana, hapana, hapana” kwa sababu katiba pendekezwa hii na ambayo naiona ni haramu ina kazi moja tu ya kulinda maslahi ya wanaccm hasa viongozi wake. 

Pia mwezi Oktoba watanzania tutakuwa na kazi nzito ya uchaguzi wa madiwani, wabunge pamoja na Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar. Sasa kuibuka kwa kikundi cha “panya road” katika muda huu wa kuelekea  chaguzi hizi kunatia  shaka juu ya usalama wa raia nchini na hasa wapinzani na wasokosoaji wa chama tawala.

Jeshi la polisi wamekuwa wanajigamba kwamba wana inteligensia kali sana na weledi mkubwa katika utendaji waowa kazi, basi sasa watuambie ukweli panya road ni nani na wanafadhiliwa na nani na kwa malengo gani? 

Kuendelea kutoa majibu mepesi kama ni wahuni tu au ni magaidi au watu wasiojulikana,  ni kuonyesha udhaifu mkubwa katika kulinda amani ya raia na mali zao na hasa katika kipindi cha kampeni za chaguzi husika ambazo tunakaribia kuzifikia. 

Lazima ifahamike wazi kwamba endapo watu watajeruhiwa na kuuawa na amani kutoweka katika chaguzi zijazo, basi ijulikane wazi kwamba Rais Kikwete na serikali yake ndiyo watakaowajibika kwa maana ndiyo wenye dhamana ya kuiongoza na kuilinda nchi yetu. 

Na ndiyo maana leo naandika na kusema bila hofu kwamba, “Jeshi la polisi acheni kuichezea amani ya Tanzania.”

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua pepe;  frmapunda91@gmail.com

No comments: