Sunday, January 18, 2015

MPANGO WA KUVUNJWA KAMATI YA MIPANGO NA FEDHA BARAZA LA MADIWANI MBINGA WAVUJA, MADIWANI WALALAMIKA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akisisitiza jambo katika moja ya vikao vyake alivyoketi hapa mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIKA hali ya kushangaza, hoja ambayo inadaiwa kupelekwa kwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga juu ya kutaka kuvunjwa kwa Kamati ya mipango na fedha ya halmashauri hiyo, imelalamikiwa na baadhi ya Madiwani wa wilaya hiyo na kuelezwa kuwa ni batili. Mtandao huu umeambiwa.

Ngaga anashutumiwa na madiwani wake kwamba, mpango huo wa kutaka kuvunja kamati hiyo amekuwa akiufanya chini kwa chini na tayari suala hilo, limefikishwa mezani kwake kwa utekelezaji, katika kikao cha baraza la madiwani kinachotarajiwa kuketi Januari 23 mwaka huu, wilayani humo.

Mpango huo umeelezwa kuwa unajidhihirisha pale mkurugenzi huyo alipovunja ratiba za vikao vya kamati husika, ambapo hata baraza hilo ilibidi liketi mwishoni mwa mwezi huu na sio tarehe hiyo, ambapo madiwani wake wameshangazwa na hali hiyo.

“Ratiba ya vikao vyote vya kamati amevivuruga na kupanga tarehe anazozitaka yeye, hata baraza hili la madiwani anataka kulifanya mapema kwa lengo la kuwakusanya baadhi ya watu wake (madiwani) ili waweze kufanikiwa mipango yao waliyojiwekea”, walisema.

Malalamiko hayo yametolewa kwa nyakati tofauti na kufafanuliwa kuwa hakuna kikao ambacho madiwani hao walikaa na kukubaliana kuvunja kwa kamati hiyo, ambayo ndio mhimili wa kamati zote za baraza la madiwani.


Walisema kitendo hicho kinachofanywa, ni mpango mchafu ambao Mkurugenzi huyo wanamtuhumu huenda amekaa na kundi lake la watu wachache, wakiwemo baadhi ya madiwani na vigogo wa halmashauri hiyo (majina tunayo) ikiwa ni lengo la kutimiza matakwa yake binafsi.

Aidha inadaiwa kuwa tendo hilo linalotaka kufanyika linatokana pia na wajumbe wachache waliomo ndani ya kamati hiyo ya mipango na fedha, kuwa mwiba kwake na kutotaka kuburuzwa wakati wa kupitisha mambo mbalimbali ya kimaendeleo ya wilaya hiyo, kinyume na taratibu husika.

 “Leo anapotaka kuvunja kamati hii maana yake ikishavunjwa, kamati zote tulizonazo ndani ya baraza hili itabidi ziundwe nyingine upya, sisi tunashangaa sana hatuja kaa kikao chochote kama madiwani na kukubaliana kupitisha maamuzi haya”, walisema.

Kadhalika waliongeza kuwa kuvunjwa kwa kamati hiyo, huenda kanuni husika za baraza la madiwani hazitaruhusu kufanya hivyo kutokana na kile walichoeleza kuwa baraza hilo linaelekea mwishoni kuvunjwa, tayari kuelekea uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu wa kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.

Hali hiyo imefafanuliwa kuwa ni vyema Mkurugenzi wa halmashauri ya Mbinga, Ngaga awemakini katika hili azingatie kanuni husika, na endapo kama zinamruhusu kufanya hivyo kabla ya yote ni muhimu akashirikisha kwanza madiwani wake, kupitia vikao halali kabla ya kuleta maamuzi katika kikao cha baraza la madiwani.

Alipotafutwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Ngaga simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa na imekuwa ni tabia yake ya kutopokea simu, na kukataa kuhojiwa au kuzungumza na waandishi wa habari hasa pale panapokuwa na malalamiko dhidi yake.

Pamoja na mambo mengine mwandishi wa habari hizi alipozungumza na Katibu wa Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo, Adolph Mandele alikiri kuwepo kwa mpango wa kuvunjwa kwa kamati hiyo ya mipango na fedha, huku akifafanua kuwa mchakato wa kutekeleza hilo unatokana na baadhi ya madiwani kuwa na tabia ya kuvujisha siri za vikao vya kamati pale vinapoketi.

Mandele alipoelezwa kwamba madiwani wenzake wanashangaa juu ya maamuzi hayo kuwa hawajashirikishwa na kubariki katika kikao husika, alikana na kusema kuwa tayari madiwani 28 walihudhuria katika kikao cha chama ambacho kiliketi kwa dharula Desemba Mosi mwaka jana, na kukubaliana kufanya hivyo.

Katibu huyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Mpapa na Katibu mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo alisema, “suala hili mimi tayari nimelifikisha kwa mkurugenzi mtendaji kwa maamuzi zaidi, nimemtaka azingatie kanuni husika za baraza ambazo zitamruhusu kufanya hivyo, kama kutakuwa kuna kanuni zinazozuia kuvunja kamati hii, jambo hili litakuwa gumu kutekelezwa na ikishindikana kabisa nitamshauri tuonyane tu ndani ya baraza kwamba madiwani hatutakiwi kutoa siri ya vikao vyetu vya kamati”, alisema.

No comments: