Saturday, January 10, 2015

TANZANIA TUIMARISHE AMANI TUSIINGIE KATIKA MACHAFUKO UCHAGUZI MKUU MWAKA HUU

Padre Baptiste Mapunda.

Na Padre Baptiste Mapunda,

MIMI siyo nabii lakini leo hii napenda kutoa maono yangu juu ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, huenda kutakuwa na uwezekano wa kumwagika damu  kutokana na usomaji wa alama za nyakati. Tukubali kwamba dunia ya leo inaogopa sana maono hasa yanayotishia madaraka ya wanasiasa wetu mufilisi.

Maono ni elimu inamhusu Mwenyezi Mungu awezaye na  ajuaye yote, hivyo basi mwanadamu kujidai anajua sawa na Mungu ni kufuru ya hali ya juu. Lakini Mungu huyo aliyemuumba mwanadamu kwa mfano na sura  yake anaweza kumfunulia mambo fulani ili aweze kuwaeleza wanadamu kuwaonya, kuwahabarisha au kuwaelekeza.

Maovu yanavyoendelea kutokea katika nchi yetu kwa  kusoma alama za nyakati najiuliza  swali moja; Je Tanzania  inakwenda kuingia katika historia ya umwagaji damu  uchaguzi mkuu wa mwaka huu? Hakika kwa maovu mengi ya nchi yetu sasa hivi ni wazi nchi haipo salama.

Nchi yetu kwa muda wa miaka mitatu sasa  imepitia  katika matukio na maovu ya ajabu ambayo yanashitua mustakabali wa  jamii  mzima, kumekuwa na mauaji   ya Albino, na utekaji wa raia wema na kujeruhi mfano Dokta Ulimboka, marehemu Dokta Mvungi, yakiwemo mauaji ya mwandishi wa habari David Mwangosi.


Taifa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaendelea kutikiswa na ufisadi wa mabilioni ya pesa za wananchi, bila hatua maalumu kuchukuliwa.

Uvunjaji wa haki za binadamu umeendelea kutokea  mara kwa mara, usalama wa raia umetikiswa mara nyingi na leo tunashuhudhia “Panya road” wakihatarisha maisha ya raia Jijini Dar es salaam, bila jeshi la polisi kuwa na uhakika Panya road ni nani hasa?

Utekaji, ukandamizaji wa vyama vya upinzani, kujeruhi na hata kuua  wanachama wao katika mikutano umeendelea kutokea na serikali kushindwa kuchukua hatua kwa wauaji hao.

Udini umeingizwa katika siasa na umewagawa waumini wa madhehebu mbalimbali kwa kupandikiza chuki.

Kulipua  Parokia ya Olasiti Arusha, mbele ya mwakilishi wa Baba Mtakatifu na kupelekea watu watatu kufa na makumi kujeruhiwa, ni alama mbaya sana  ya kuelekea  umwagaji damu katika nchi yetu.

Wizi wa mabilioni ya pesa EPA, Richmond, Kagoda, na sasa Escrow ni alama ya kukosekana kwa amani. Kwa matukio niliyoonyesha hapa ni wazi  Tanzania  sasa inaelekea  kumwaga damu hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2015. 

Nasema sasa kwa uwazi na uhuru ili serikali ya CCM isipate kisingizio kwamba haikujua, sasa inajua kwamba kinachoendelea ni maandalizi ya vurugu, maasi, chuki, fitina na maafa kwa wananchi.

Uchaguzi wa serikali za mitaa ni alama tosha ya umwagaji damu ninayozungumzia katika makala haya, uchaguzi huo haukuandaliwa vizuri na mwishowe ni kuibeba ccm kwa mabavu na mabomu. Je huku si kuandaa maafa wakati wananchi wanajua  umuhimu wa kupiga kura yao?

Matokeo yake  uchaguzi uligubikwa  na kasoro lukuki, fitina, mizengwe, upendeleo, ubaguzi, vitisho, kujeruhiwa  na hata wengine kuuawa. Je hii ndiyo amani  inayohubiriwa na ccm kila kukicha?

Pamoja na maeneo mengine chama hiki cha mapinduzi  kushindwa, lakini  ubabe bado unaendelea kuonyeshwa kwa kuwatangaza wanaccm walioshindwa na hata kulazimisha  waapaishwe. Je nani anahatarisha amani ya nchi  wapinzani au wanaccm? Na sisi viongozi wa dini tuhubiri amani ipi sasa?

Sasa hivi wanatengeneza machafuko kupitia uchaguzi mkuu  utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu. CCM lazima wajue kwamba gharama ya uchakachuaji wa kura ni machafuko, vita na maafa kama yalivyotokea nchini Kenya katika ushindi uliochakachuliwa na tume ya  marehemu Kivuitu mwaka 2007.

Uchakachuaji  huo ulisabaisha wananchi kuyakataa matokeo ya ushindi huo. Serikali yetu inatupeleka wapi?

Ni vema tutafakari kwani enzi hii ni tofauti na miaka ya 2000, 2005, na hata 2010 wananchi wamebadilika. Sasa hivi Watanzania wameamka wanataka mabadiliko kama alivyoasa Mwadhama Kardinali Pengo,  kwamba Tanzania  ilipofikia sasa inahitaji mabadiliko ambayo yataletwa na watu maskini kwa kuungana ilikuwang’oa  viongozi  mafisadi. CCM lazima ijue  sasa mabadiliko hayaepukiki kamwe.

Lazima watambue kwamba enzi ya kuamini kwamba ndiyo chama pekee na kwamba bila ccm Tanzania haiwezekani  zimeisha sasa. CCM imelewa madaraka, ccm imetekwa  nyara na mafisadi kama alivyoasa  Mwadhama Kardinali Pengo katika  sherehe ya kuzaliwa kwake. 

Uchaguzi mkuu wa mwaka huu ccm watajaribu kutumia kila mbinu ili kuendelea kubaki madarakani. Watatumia pesa  kununua kura, watatupatia khanga, kofia, pilau, kuahidi vyeo, watatumia wanahabari, watatumia viongozi wa dini na udini, lakini haitasaidia kitu. 

CCM watatumia vyombo vya dola vikiwamo vya ulinzi na usalama, polisi, FFU, Usalama wa taifa na hata Jeshi la wananchi, lakini havitasaidia, kwa sababu muda wa mabadiliko umefika.

Wapinzani watauawa na wapenda mabadiliko na maendeleo ya nchi, watu watabambikizwa kesi hasa wapinzani, kura zitaibiwa, matokeo yatabadilishwa, na walioshindwa watatangazwa  washindi lakini yote hayo hayataiokoa kutoka katika kaburi la kifo. 

Kitakachoikoa chama cha mapinduzi ni kukubali matokeo, na kuanzia sasa ni kuunda tume huru ya uchaguzi, kuboresha daftari la wapiga kura, kurekebisha sheria na kanuni mbovu za  uchaguzi na kuwa na wasimamizi watenda haki kwa wote.

Nawaomba viongozi wa dini wasaidie kuiepushe nchi ili isitumbukie katika machafuko, vita na hatimaye mauaji kama yalivyotokea nchini Kenya mwaka 2007. Maono yangu  yanatokana na kusoma alama za nyakati  ni kwamba  serikali ya ccm isipoangalia  itaiingiza nchi katika umwagaji wa damu kupitia uchaguzi  mkuu wa mwaka huu 2015.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua pepe;  frmapunda91@gmail.com

No comments: