Thursday, January 1, 2015

SCCULT YAINGIA KATIKA KASHFA MPYA, YADAIWA KUKUMBATIA FEDHA ZA WAKULIMA



Kassian Nyandindi,
Songea.

OFISI ya Chama Kikuu Cha Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT) mkoani Ruvuma, imeingia katika kashfa mpya baada ya uongozi wa chama cha kuweka na kukopa, Kihulila juu SACCOS wilaya ya Mbinga mkoani humo, kuishushia lawama kwamba imeshindwa kushughulikia lalamiko lao kwa muda mrefu la kurejeshewa, shilingi milioni 3,122,000 baada ya kujitoa uanachama miaka mingi iliyopita.

Walisema licha ya ofisi hiyo kuwa na taarifa kamili juu ya jambo hilo na ufuatiliaji wa madai hayo, kuanza kufanyika tokea Februari 16 mwaka 2010 na SACCOS hiyo ilipojitoa uanachama kwa hiari, Desemba 30 mwaka 2008 hakuna jitihada zilizozaa matunda mpaka sasa.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake Katibu wa idara ya mikopo Kihulila juu SACCOS, Kelvin Ndunguru alisema kawaida tokea siku walipojitoa uanachama, baada ya siku 90 ilibidi SCCULT warejeshe mafao yao yaliyotokana na michango mbalimbali waliyokuwa wakichangia.

Ndunguru alifafanua kuwa tatizo hilo lipo hata mezani kwa Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani humo, na viongozi wengine wa wilaya ya Mbinga, lakini hakuna majibu sahihi wanayopewa juu ya madai hayo huku siku zikiendelea kupita.


Vilevile alieleza kuwa wanachama wa SACCOS hiyo hawauelewi uongozi wa ushirika uliopo madarakani mkoani Ruvuma, juu ya mwenendo wa suala hilo unavyotekelezwa huku wakidai kwamba fedha zao zipo nje ya chama chao kwa muda mrefu jambo ambalo, linasababisha kuzorota kwa maendeleo yao na chama kwa ujumla.

“Mpaka nafikia hatua ya kukaa na wewe kukueleza jambo hili, bodi ya uongozi wa chama chetu cha kuweka na kukopa tulikaa kikao na kuridhia malalamiko yetu haya tuyafikishe hata kwenu waandishi wa habari, ili kilio chetu serikali ikisikie na kukifanyia kazi huenda tukapata haki yetu ya msingi kwa sababu tumelalamika maeneo mengi hakuna tuliposikilizwa”, alisema.

Alisema kuwa pamoja na kuandika barua nyingi za kukumbusha juu ya suala hilo na kuzipeleka katika ofisi husika (nakala tunazo) wanaiomba serikali, kupitia Wizara yake ya kilimo chakula na ushirika kuingilia kati ili waweze kupata fedha zao ambazo wanaendelea kudai miaka mingi sasa imepita.

Pamoja na mambo mengine, gazeti hili inayo barua yenye kumbukumbu namba SCCULT/RUR/KHJ/VOL 1/31 ya Februari 23 mwaka 2012, yenye kuonyesha inatoka kwa Meneja mkuu wa mkoa wa Ruvuma (SCCULT) ikikiri kudaiwa madai hayo na Kihulila juu SACCOS huku nakala ikipelekwa kwa Katibu mtendaji wa chama hicho kikuu cha akiba na mikopo Tanzania na Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani humo kwa utekelezaji zaidi, jambo ambalo limekaliwa kwa  muda mrefu huku likiendelea kuleta sintofahamu miongoni mwa wanachama.

Barua hiyo ambayo inakubaliana na madai hayo inasema, “ni kweli kwamba Kihulila juu SACCOS ilikuwa mwanachama na mshiriki mzuri wa maazimio ya mikutano mikuu ya SCCULT na iliamua kujitoa uanachama wa hiari, kwa barua ya kwanza ya Desemba 30 mwaka 2008,

“Kufuatia maombi hayo ya kujitoa uanachama katika mkutano mkuu wa SCCULT uliofanyika mkoa wa Mtwara, Februari 16 mwaka 2010 waliridhia ombi hilo “, inasema barua hiyo. 

Aidha uchunguzi umebaini kuwa kwa kuzingatia sheria ya ushirika baada ya wanachama kuridhia kujitoa uanachama, SCCULT walikuwa na wajibu wa kuandaa malipo stahiki ya SACCOS hiyo kwa mchanganuo ufuatao; ambapo Akiba na faida ya juu ilikuwa walipe shilingi milioni 2,717,080.00, Hisa shilingi 345,000.00 na Ada ya mkopo ilikuwa shilingi 60,000.00 na kufanya jumla kuu ya deni wanalodaiwa kuwa ni shilingi milioni 3,122,080.00.

Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma, Fausta Kasuga hakuweza kupatikana ili aweze kutolea maelezo ya kina juu ya madai hayo ya chama cha kuweka na kukopa, Kihulila juu SACCOS kilichopo wilayani Mbinga.

Hata hivyo jitihada ya kumpata Meneja wa mkoa wa Ruvuma, wa Chama Kikuu Cha Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT) Hezron Luvanda kwa njia ya simu ili naye aweze kuzungumzia malalamiko hayo, zilifanikiwa ambapo alikiri juu ya wanachama wa SACCOS hiyo kudai fedha hizo.

Luvanda alisema “mimi nimekwisha acha kazi sipo Ruvuma, na ofisi yetu hapo imefungwa siku nyingi, hakuna mtu wakuweza kukupatia ufafanuzi juu ya jambo hili”.

No comments: