Thursday, January 15, 2015

WADAU WA ELIMU WALIA NA SERIKALI, KATIBU MKUU TAMISEMI AWASHANGAA NA KUWALAUMU MADIWANI WA MBINGA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Na Kassian Nyandindi,

Ruvuma.

BAADHI ya Madiwani na Wadau wa elimu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuacha kufumbia macho tatizo la mgogoro uliopo kati ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hussein Ngaga na baadhi ya watumishi wake wa idara ya elimu msingi huku wakieleza kuwa hatua zisipochukuliwa mapema huenda wilaya hiyo ikarudi nyuma kimaendeleo, hususani katika sekta ya elimu ambayo wilaya inaonekana kwa sasa ikifanya vizuri.

Wadau hao wameinyoshea kidole ofisi ya TAMISEMI wakidai kuwa, imekuwa ikimbeba Mkurugenzi huyo licha ya matatizo yaliyopo hapa wilayani kuwafikia.

Aidha walisema kuwa Ngaga amekuwa chanzo cha migogoro kazini, ambapo muda mwingi haelewani na baadhi ya watumishi wenzake, hususani wa idara ya elimu msingi.

Imedaiwa kuwa matatizo hayo yapo mezani kwa viongozi wa TAMISEMI ikiwemo hata kwa Katibu Mkuu, Jumanne Sagini lakini wanashangaa kuona kutochukua hatua madhubuti ikiwemo kumwajibisha mkurugenzi huyo, ambaye sasa amekuwa kero kwa madiwani hao na wananchi wa wilaya hiyo.

Walisema ni wakati sasa kwa ofisi hiyo kuchukua hatua na sio kukaa kimya, ukizingatia kwamba kilio cha wanambinga juu ya kukerwa na migongano kazini ambayo anaiendekeza mkurugenzi huyo, imedumu kwa muda mrefu.


Hivi sasa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, imekuwa ikiyumba kimaendeleo hususani katika sekta ya elimu ya msingi ambapo mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo Ngaga analalamikiwa na madiwani wake kuchukua hatua ya kumsimamisha kazi afisa elimu msingi, Mathias Mkali bila kuzingatia taratibu za kiutumishi wa umma ikiwemo hata baraza lake la madiwani lililoketi mara ya mwisho, Oktoba 27 mwaka jana halikumtuma afanye hivyo.

Nimezungumza na baadhi ya Madiwani wa wilaya hiyo walisema, Ngaga amekuwa akichukua maamuzi peke yake kwa kudharau maagizo yanayotolewa na baraza la madiwani kupitia vikao halali, na hata wakati mwingine amekuwa akifikia hatua ya kubadilisha mihtasari ya makubaliano husika ya vikao vya kamati mbalimbali, kwa malengo yake binafsi.

Walisema hivi karibuni kamati za madiwani ambazo zimekuwa zikiketi katika vikao vyake, wajumbe wameshangazwa na mkurugenzi huyo muda mwingi baadhi ya mambo yaliyokuwa yamejadiliwa na kujenga makubaliano, yeye huyabadilisha na kuweka mambo tofauti na makubaliano husika hatimaye ndani ya vikao husababisha kurushiana maneno na watu kujengeana chuki pasipokuwa na ulazima.

Ambapo walitolea mfano kuwa, katika kikao walichoketi Novemba 25 mwaka jana cha kamati ya mipango na fedha, Ngaga alileta muhtasari kwa kamati hiyo ambao ulikuwa ukieleza kuwa Waratibu elimu kata haikupitishwa na baraza kwamba wapewe mafuta, jambo ambalo wajumbe walimshangaa na kumweleza sio kweli bali baraza hilo lilikubaliana wapewe ili waweze kuweka kwenye pikipiki zao, ziwarahisishie waweze kufanya ufuatiliaji wa mazoezi ya mitihani kwa wanafunzi wa darasa la saba katika kata husika, ikiwa ni lengo la kuboresha taaluma wilayani humo.

“Baada ya mkurugenzi huyu kumkosoa kwenye jambo hili alionekana kuwa mkali huku akitutishia kwa maneno makali na kulazimisha tupitishe mambo anayoyataka yeye, mjumbe mwenzetu mmoja aliamua kutoka nje ya kikao baada ya kushindana kwa muda mrefu na kutofikia muafaka”, walisema.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga alipotafutwa ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya madai hayo, hakuweza kupatikana na simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa na imekuwa ni tabia yake ya kutopokea simu, na kukataa kuhojiwa au kuzungumza na waandishi wa habari pale panapokuwa na tatizo katika halmashauri hiyo.

Alipoulizwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Jumanne Sagini juu ya ofisi yake kama inalifahamu suala hilo kama madiwani hao na wadau mbalimbali wa elimu wanavyodai alisema, kuhusiana na madai kwamba ofisi yake inambeba mkurugenzi huyo alikana huku akiongeza kuwa endapo anasikia kama kuna mtumishi yeyote wa serikali za mitaa ambaye anakiuka maadili ya utumishi wa umma, yupo tayari kumwajibisha kwa namna moja au nyingine.

Pamoja na mambo mengine alionyesha kushangaa na kuwalaumu madiwani wa Mbinga na kusema kuwa, wao ndio wenye rungu na mamlaka kupitia vikao vyao baraza la madiwani, wanaweza kumwajibisha mkurugenzi huyo pale wanapoona anakosea na kuipeleka wilaya yao vibaya tofauti na maadili ya utumishi wa umma.

“Nakuambia ofisi yangu haiwezi kumuacha mtumishi wa namna hiyo, hao wanaosema kwamba mkurugenzi wa Mbinga mimi nambeba sio kweli, nikibaini kuna mtumishi anayekiuka taratibu husika nitambamiza tu, siwezi kumuacha na sijawa na mtu ambaye ninambeba”, alisema Sagini.

Kadhalika alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya ofisi yake kama inafahamu juu ya matatizo haya yanayoendelea sasa wilayani Mbinga, alisema hana nafasi ya kuweza kuongea kwa muda mrefu kutokana na kubanwa na vikao huku akimtaka mwandishi wetu, ampigie kwa muda mwingine ili aweze kutolea ufafanuzi zaidi.

“Ndugu yangu nakutakia siku njema, naomba nitafute leo majira ya saa 10 tuweze kuzungumza zaidi juu ya jambo hili, hapa nilipo naingia kwenye kikao nimebanwa kwa kweli, aliishia kukata simu”, alisema.

No comments: