Thursday, January 29, 2015

BABA KANUMBA: NILIMTEMEA MATE KABROTHER AWEZE KUFANIKIWA KATIKA KAZI ZAKE

Msanii wa filamu nchini, Senga upande wa kulia akiwa na msanii mwenzake katika picha ya pamoja, Gidion Kabrother.
Na Kassian Nyandindi,

Ruvuma.

CHARLES Kanumba ambaye ni baba wa aliyekuwa nguli wa filamu hapa nchini, Marahemu Steven Kanumba amefunguka akisema kuwa alimtemea mate msanii Gidion Simon maarufu kwa jina la Kabrother, ili aweze kufanikiwa katika kazi zake za uigizaji wa filamu kama alivyokuwa mwanae Kanumba.

Alisema aliamua kufanya hivyo, ili ikiwezekana amrithi mwanae huyo ambaye alikuwa ni rafiki yake kipenzi akishirikiana na mwanae, katika kazi za uigizaji wa filamu kwa muda mrefu.

“Nilimtemea mate huyu mtoto, kwa sababu katika kazi zake alikuwa mtu wa karibu sana na mwanangu wakishinda hapa nyumbani, hivyo niliona nifanye hivi niweze kumpatia baraka na Mungu akimbariki aweze kuonyesha maajabu kama mwenzake”, alisema.

Alifafanua kuwa, Kabrother wakati anaanza kazi zake za uigizaji alikuwa akijifunza kupata ujuzi wa fani hiyo, kutoka kwa marehemu Kanumba.

Hayo yalisemwa na Baba Kanumba, wakati alipokuwa akizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu ambapo aliongeza pia kwa kuwataka waigizaji wa filamu hapa nchini, kuwa na ushirikiano katika kazi zao ili waweze kusonga mbele katika tasnia yao ya sanaa na maigizo ya aina mbalimbali.

“Namsifu Kabrother kwa juhudi anazozifanya, ameanza kazi hii kwa muda mrefu mpaka hapa alipofikia katika kukuza kipaji chake”, alisema Baba Kanumba.


Jitihada ya kumpata Gidion Kabrother ili aweze kuthibitisha hilo alisema; “ni kweli baba Kanumba alinitemea mate, hii ni baraka yake ambayo alinipatia niweze kufanikiwa katika kazi zangu, nategemea Mungu atanisaidia”.

Pamoja na mambo mengine msanii huyo wa filamu alikiri pia kuwa rafiki wakaribu na marehemu Kanumba, huku akieleza kuwa hata katika kazi zake walikuwa wakishirikiana kwa pamoja.

Kabrother hivi sasa anatarajia kutoa filamu yake mpya yenye picha kali, ambayo itatamba kwa jina la Mkuki kwa Nguruwe hivyo wadau mbalimbali amewataka kukaa mkao wa kula na kuipokea albamu hiyo, kwa kuendelea kumuunga mkono kwa kazi zake.

Filamu hiyo inaiasa jamii hasa kwa wale wenye kipato, kuacha tabia au matendo ya kuumiza wenzao kwa namna moja au nyingine kutokana tu, na hali ya uchumi mzuri walionao.

Kabrother uzoefu wake katika fani ya uigizaji wa filamu hapa nchini, amepitia kwenye vikundi vya sanaa vya Tamacaefo sunlight (Manyoni), Emima (Morogoro) na Best tallent (Shinyanga).

Kwa sasa anafanya kazi zake za usanii kwa kushirikiana na wasanii wakongwe hapa nchini Senga, Pembe, Kinyambe na Matumaini na kwamba Kabrother anatamba na filamu zake tatu ambazo tayari zipo sokoni zenye kufahamika kwa majina ya Exccident, Nimeshindwa na ile iitwayo Ni shidaa.

Pamoja na mambo mengine Gidion Kabrother licha ya kuwa msanii, pia ni mwalimu wa shule za msingi ambaye amebobea kwenye masomo ya Hisabati, Kingereza na Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).

Kadhalika ni mtaalamu wa michezo ya mpira wa mikono (Hand ball) na mpira wa wavu (Volley ball), na kwamba kwa mtu yeyote yule ambaye anahitaji kupata filamu zake anaweza kufanya mawasiliano kwa kupiga simu ya kiganjani namba; 0757 947301.





No comments: