Friday, January 2, 2015

BREAKING NEWS: MBINGA WATOTO WANUSURIKA KIFO BAADA YA KUTOKEA MLIPUKO WA KITU CHENYE NYAYA NYINGI

Hapa ni Jalalani karibu na shamba la mahindi mtaa wa Kiwandani Mbinga mjini mkoani Ruvuma, ambako watoto sita waliokota kifaa chenye nyaya nyingi, ambacho baadae kiliwalipukia na kuwajeruhi.

Mtoto Emmanuel Mwingira (7) akiwa amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, baada ya kulipukiwa na kitu kilichokuwa kimetengenezwa na nyaya nyingi wakati alipokuwa akicheza na wenzake na kusababisha kuumia mkono wake wa kulia, na sehemu mbalimbali za mwili wake.
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

WATOTO wanne kati ya sita wamenusurika kifo, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma baada ya kuwalipukia kitu ambacho kimeunganishwa na nyaya nyingi na kuwajeruhi vibaya, wakati mwenzao mmoja akiwa amekishika anaunganisha nyaya hizo walipokuwa wanacheza pamoja. 

Taarifa za awali ambazo zilisambaa mjini hapa, ilielezwa kuwa mlipuko huo ulitokana na kitu ambacho kilizaniwa kuwa ni bomu ambalo limetengenezwa kienyeji, jambo ambalo sio kweli.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela, ambaye alikuwa eneo la tukio alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alithibitisha kuwa, tukio hilo limetokea leo majira ya saa 5:00 asubuhi katika mtaa wa Kiwandani mjini hapa, wakati watoto hao wakiwa wanachezea kitu ambacho kilikuwa kimeunganishwa na nyaya nyingi.

Msikhela alikitaja kitu hicho kuwa ni kilipuzi ambacho hupenda kutumika na watafiti wa madini migodini au walipuaji baruti, huku akieleza kuwa tukio hilo ni la bahati mbaya ambapo liliwakumba watoto hao baada ya kuokota kifaa hicho jalalani.


Aliwataja watoto waliolipuliwa kuwa ni Philiberth Mbungu (10), Augustino Millanzi (5), Geofrey Ndunguru (8) na Emmanuel Mwingira (7) ambao wote wameumizwa sehemu mbalimbali huku wengine wawili Ayubu Methew (10) na Hassan Mapangi (5) wakiwa na majeraha ya kawaida mwilini.

Mwandishi wetu ambaye alitembelea katika eneo la Hospitali ya wilaya ya Mbinga, na kuzungumza na Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Elisha Robert alifafanua kuwa mtoto Philiberth na Augustino wamekimbizwa katika hospitali ya mkoa Songea kwa matibabu zaidi.

Alisema watoto hao wamepelekwa huko kutokana na kujeruhiwa vibaya sehemu za usoni machoni, ambapo alieleza kwamba kuna vipande vidogo vidogo vya vyuma vimeingia ndani yake.

“Niliamua kuchukua hatua ya kuwapeleka hospitali ya mkoa ili wakapatiwe matibabu zaidi, kutokana na jinsi nilivyowaona hali zao sio nzuri na mimi nipo kwa karibu sana naendelea kufuatilia kujua hali zao zipoje lakini taarifa nilizonazo tayari wamepokelewa na wanahudumiwa”, alisema Robert.

Kadhalika aliongeza kuwa Geofrey na Emmanuel wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Mbinga, ambapo nao wamejeruhiwa usoni na mikononi na hali zao zinaendelea vizuri.

Awali Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema uchunguzi unaendelea kufanyika juu ya tukio hilo, na kwamba alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuwa waangalifu na watoto wasiwaache wakitembea hovyo, hivyo pale wanapoona kitu chenye muunganiko wa nyaya wasikiguse badala yake watoe taarifa haraka kwenye vyombo vya usalama ambavyo vipo karibu nao.


No comments: