Monday, January 5, 2015

VIONGOZI WA DINI TANZANIA BADILIKENI MWAKA 2015

Na  Padre Baptiste Mapunda,

NIMEANDIKA mara nyingi sana juu ya wajibu wa viongozi wa dini katika jamii. Hao ni viongozi wa dini lakini pia hawawezi kusahau kuwa ni viongozi wa jamii ambao wanaaminiwa na watu wengi sana.

Viongozi wa dini ni wadau wakubwa sana katika suala nzima la ujenzi wa demokrasia, hakiza za binadamu, maendeleo ya nchi, na utawala bora lakini kubwa zaidi viongozi hawa lazima  wahamasishe  uhuru  wa mawazo  pamoja na kuutetea ukweli na haki sawa hasa kwa wanyonge.

Mimi sitegemei kiongozi kuwa mwoga wa kusema ukweli pale ambapo serikali inapokosea halafu viongozi wa dini tunageuka kuwa wanafiki. Hii siyo injili ya Yesu Kristo na siku zote injili ya Yesu inasema  viongozi wa dini ni manabii katika jamii.

Mwaka huu 2015 ni mwaka wa pekee sana katika nchi yetu kwa sababu ya matukio muhimu hasa ya uchaguzi mkuu na upitishwaji wa katiba inayopendekezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ninayoiita katiba haramu ya CCM.

Kutokana na masuala hayo na makando kando yake kama umuhimu wa kuunda tume huru ya uchaguzi, uandikishwaji na uboreshwaji wa daftari la wapiga kura, viongozi wa dini wanamezewa mate mengi sana na wanaccm kuona kama watakuwa upande wao au wa wapinzani, au watabaki katikati kutafuta maslahi ya jamii.

Kama alivyosema Mwadhama Cardinali Pengo katika sikukuu ya kusherehekea miaka 70 ya uhai wake kwamba tulipofikia kama nchi sasa tunahitaji mabadiliko. Alikwenda mbali zaidi nakusema kwamba mabadiliko haya yataletwa kwa kuunganisha nguvu za watu maskini ili kuwaondoa viongozi matajiri waliopo madarakani.



Viongozi waliopo madarakani ni wa CCM ambao wanaunda serikali yenye mamlaka. Na watanzania tumeshuhudia  wizi wa mali wa mabilioni ya pesa kuanzia Richmond, Epa, Kagoda, Rada na sasa Escrow wizi huo unawahusisha hasa viongozi wa serikali hii  na hili linadhihirishwa na kufukuzwa kwa  mawaziri na watendaji wengine wa serikali kama vile Mwanasheria mkuu.

Katika hili inaonekana kama serikali hii ya chama tawala kazi yake kubwa ni kulinda na kutetea wezi wa mali ya umma. Je, viongozi wa dini hatuelewi hilo au tunajifanya tunaishi katika dunia nyingine? Kwa mantiki hiyo mimi nashangaa sana  ninaposikia makongamano ya kuombea amani lakini ndani yake mnawachomeka  viongozi wa serikali  waje kuzindua, mimi  naona hii ni dhihaka kwa Mungu.

 Wakati viongozi hao hao wa serikali ndiyo wanaoharibu amani kwa kutumia polisi na vyombo vingine vya ulinzi halafu wanaalikwa  kushiriki katika makongamano ya kuombea amani haingii akilini   na rohoni mwangu. Hii ni kufuru mbele ya mwenyezi Mungu ajuaye yote yaliyo moyoni mwetu.

Tunapoanza mwaka huu wa 2015 natoa wito  wangu  kwa viongozi wa dini na waumini kuacha kutetea dhuluma zinazofanywa na serikali ya CCM dhidi ya raia. Viongozi wa dini kuacha kuombea amani  wakati  serikali inaendelea kupora  pesa na rasilimali za wananchi bila aibu wala hofu na kuvunja haki za binadamu, kwa kutumia polisi na vyombo vingine vya ulinzi.

Viongozi wa dini  nawashauri acheni kutumiwa na utawala huu wa chama hiki kuitisha  mikesha ya maombi ambayo  hayazai matunda. Tangu mikesha hiyo ianze na viongozi wa serikali kuhudhuria mbona hakuna mabadiliko? Wizi wa mali ya umma unaendelea, polisi wanazidi kuua raia hovyo, ukandamizaji, matusi na kejeli kwa viongozi wa dini, acheni kununuliwa nyie ni viongozi wa dini.

Namna nyingine mimi napendekeza mikesha hiyo  iwe ni fursa ya kulaani  vitendo dhalimu vya serikali ya CCM, ili watambue kwamba  wanachofanya si kizuri. Viongozi wa dini muwe na ujasiri wa kuikemea serikai hii ili iache kuendekeza mfumo wa kuendesha serikali kwa manufaa ya chama na siyo wananchi maskini wa Tanzania.

Viongozi wa dini mna nafasi nzuri sana ya kukemea maovu ya serikali yanayokiuka  haki za binadamu   kwa raia wake, Mimi nakumbuka kule Kenya kipindi cha utawala wa Rais Moi chini ya KANU kulikuwa na unyama mwingi sana ukiendeshwa na KANU, lakini viongozi wa dini walifunguka  wakakemea kwa nguvu na akili zote.

Viongozi wa dini zote waliungana walipaza sauti zao kama alivyosema Cardinali Pengo  kwamba wasiposikia  basi mawe yatasikia. Hatimaye waumini wote nao bila kujali dhehebu wakaungana na wananchi kupitia sanduku la kura wakaiondoa KANU madarakani na  ikazikwa katika kaburi ka kusahaulika  ipumzike kwa Amani (R.I.P).

Kanisa la Romani kwa mfano lilimwandikia Rais Moi, barua ya kumwelezea jinsi maovu yaliyokuwa yanaendeshwa na wakuu wa Wilaya, Mikoa, Usalama wa taifa, Polisi kwa jina lake bila kumwogopa.  Ukweli  na uhuru ulitawala mioyoni mwa viongozi wa dini hapakuwa tena  na muda wa kuogopa kufa.

Viongozi wa madhehebu mengine walifungwa jela kwa sababu ya kutetea wananchi kama mchungaji Tom Njoya wa kanisa la Presbyterian. Naye  Askofu wa dhehebu la Anglikan aitwaye Alexander Muge aliiambia serikali ya Moi kwamba kanisa linawajibu wa kupinga haki  za binadamu zilizotoka kwa Mungu na uhuru vinapovunjwa na lazima tuwatetee wanyonge wasio na sauti.

 Hii ni mifano michache tu ninayoikumbuka, lakini ipo mingi kama ya Askofu mkuu mstaafu  wa Jimbo Kuu la Nairobi, Mwananzeiki Ndingi ambaye alikuwa mwiba kwa uongozi wa KANU.

Mjadala wangu huu  haulengi kujenga chuki na uhasama na viongozi wa serikali ya Chama cha mapinduzi kama wengi watakavyofikiria, bali ni wajibu wa viongozi wa dini   kuionyesha  serikali kwamba, sasa imefika mahali imepotoka katika utendaji wake.

Nakumbuka enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere alikuwa anapenda kukutana na viongozi wa dini na kupata ushauri, kwa kweli alikuwa nao karibu sana na hivi aliweza kuelewa  walikuwa wanaionaje serikali yake na hivi kujirekebisha.

Lakini serikali ya awamu ya nne naona imefanikiwa kujiweka mbali na viongozi wa dini na hivi kuendelea na sera zake za ufisadi, dhuluma, na vitisho kwa wananchi wake bila kuwa na hofu ya Mungu. Viongozi wa serikali kuongoza nchi bila kuwa na hofu ya Mungu ni janga na hapo ndipo tulipofikia Tanzania  kubaki nchi ya dhuluma  na udhalimu kwa wananchi wake.

Kuendelea  kuandaa mikesha ya kuombea amani na kuwaalika viongozi wa serikali kunaijengea kiburi serikali hii ya chama hiki tawala, kwamba  bado inakubalika na kwamba  hakuna tatizo lolote nchini kitu ambacho siyo kweli na hii ni alama ya upofu wa kiuongozi na ulevi wa madaraka.

Lakini kuna wakati inatupasa kuipa serikali kiashirio kwamba sasa mmepotoka katika utendaji wenu, hivi nasi tunawaacha kwa sababu  tutakwenda kinyume na injili ya Bwana.  Hata Mungu alipobaini mfalme fulani anakiburi na hasikii basi aliachana naye na huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.

Nimalize tu kwa kusema kwamba viongozi wa dini lazima mjue na kutambua kwamba Tanzania ya sasa iliyojaa  ufisadi, rushwa, uonevu wa kila aina, dhuluma, ujangili, wizi wa mali ya umma, uporaji wa meno ya tembo, utekaji, utesaji, utoboaji macho, ukwapuaji wa kucha kwa koleo, mauaji ya polisi, wizi wa kura, uvunjaji  wa haki za binadamu, ubambikizi wa kesi, matusi na kejeli.

Ili kupambana na maovu hayo nchi hii  inahitaji viongozi wa dini wenye ujasiri wa kukemea maovu hayo kwa uwazi bila kuogopa. Lazima ifike mahali viongozi wa dini kama kule Kenya  wawe jasiri kama Yohani mbatizaji aliyekatwa kichwa kwa kukemea uzinzi wa mfalme Herode.

Maana yake hapa ni pana hivyo hakuna  mageuzi, mabadiliko na mapinduzi yasiyo na sadaka pengine hata kufa kwajili ya mapinduzi hayo.  Viongozi wa dini bila kuchochea  chuki, vurugu na maafa kama serikali inavyopenda kutumia propaganda ya Rwanda ifike mahali tusimame kidete kutetea wananchi maskini kwa kusema SASA IMETOSHA na siku hiyo itakuwa mwanzo wa mageuzi.

Ukombozi wa Tanzania kutoka mikononi mwa CCM unategemea sana mwamko wa viongozi wa dini nchini. Je, mmeanza kuamka?

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua pepe; frmapunda91@gmail.com

No comments: