Wednesday, November 1, 2017

WASIOSHIRIKI KUFANYA USAFI SONGEA KUTOZWA 50,000

Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema akiwa katika mtaa wa Mwinyi mkuu moyo uliopo katika Manispaa ya Songea akihamasisha zoezi la kufanya usafi katika mitaa mbalimbali mjini hapa.
Na Albano Midelo,   
Songea.

MKUU wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Palolet Kamando Mgema amemtaka Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Songea mkoani humo kwa kushirikiana na maafisa wake wa afya, kuwahimiza wananchi katika Manispaa hiyo waweze kushiriki kikamilifu kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kufanya usafi katika maeneo ya umma.

Aidha alisisitiza kuwa kwa yule mwananchi ambaye hatashiriki katika siku hiyo maalum ya kufanya usafi achukuliwe hatua ikiwemo kutozwa faini ya shilingi 50,000.

Mgema alitoa agizo hilo juzi wakati alipokuwa katika mtaa wa Mwinyi mkuu moyo uliopo katika kata ya Majengo mjini hapa, huku akishirikiana na wananchi wa mtaa huo kufanya usafi wa Mazingira.


Alisema kuwa sheria ya usafi wa mazingira inawatia hatiani wale wote waliosababisha kuwepo kwa uchafu katika eneo husika na wale wanaokataa kufanya usafi adhabu yake ni faini ya shilingi 50,000.

Kadhalika aliwaagiza Watendaji wa mitaa waliopo katika Manispaa ya Songea kuwaandika majina wananchi wanaoshiriki usafi huo kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi na kwamba kwa wale ambao hawashiriki watozwe faini na ofisi yake ipelekewe taarifa haraka ni wangapi wamelipa fedha kutokana na kupigwa faini ya kutoshiriki katika kufanya usafi wa mazingira.

Mgema amezitaka kaya zote zinazoishi katika mitaa 95 iliyopo kwenye Manispaa hiyo kuchangia mchango wa usafi wa mazingira ambao ni shilingi 2,000 kila mwezi.

“Usafi wa mazingira ni jambo la lazima ili tuweze kukabiliana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama vile kipindupindu na malaria”, alisisitiza.


Hata hivyo alisema katika nchi zilizoendelea hakuna watu wanaougua magonjwa yanayotokana na uchafu kutokana na kuzingatia masuala ya usafi na kwamba nchi hizo zinashangaa kuona kuna watu wanaugua na kufa kutokana na magonjwa ya uchafu.

No comments: