Thursday, November 9, 2017

DOKTA MAGUFULI ATENGUA UTEUZI MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI TUNDURU

Na Mwandishi Wetu,

RAIS Dokta John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Abdallah Mussa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi wilayani humo.

Kutenguliwa kwa uteuzi wa Mkurugenzi huyo leo Alhamisi Novemba 9 mwaka huu kumefanyika siku tatu baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa wakurugenzi wengine wawili.

Taarifa ya Rebecca Kwandu, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini katika Ofisi ya Tamisemi imesema kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mussa Iyombe ndiye aliyotoa taarifa ya kutenguliwa kwa uteuzi huo leo mjini Dodoma.


Alisema kwamba kutokana na hatua hiyo uteuzi wa Mkurugenzi mwingine utafanyika hapo baadaye.

Rais Magufuli Novemba 6 mwaka huu alitengua uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za Manispaa ya Bukoba, Erasto Mfugale na wa Halmashauri ya Bukoba, Mwamtumu Dau.

Viongozi hao walishindwa kutaja kiasi cha fedha za Mfuko wa Barabara zilizopokelewa kwenye halmashauri zao walipoulizwa na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba.

Alipoitwa mbele na kutakiwa kutaja kiasi halisi cha fedha zilizopokelewa katika halmashauri kwa ajili ya mfuko huo, Mwantumu alijibu kuwa ana idara nyingi anazozisimamia hivyo isingekuwa rahisi kwake kukumbuka kila kitu, hivyo ni mpaka awepo mweka hazina huku akiongeza kuwa hawezi kusema uongo.


Dokta Magufuli katika mkutano huo alisema kuwa amewasamehe lakini baadaye Ikulu ilitoa taarifa ikieleza Rais ametengua uteuzi wao.

No comments: