Wednesday, November 1, 2017

MANISPAA SONGEA YAANZA KUTOKOMEZA MAZALIA YA MBU

Na Albano Midelo,   
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imeanza rasmi upuliziaji wa dawa kwa ajili ya kuua mazalia ya Mbu katika mitaa iliyopo kwenye kata 21 zilizopo ndani ya Manispaa hiyo.

Afisa afya wa Manispaa ya Songea, Vitalis Mkomela alisema kuwa zoezi la upuliziaji lilianza Oktoba 19 mwaka huu katika mitaa ya kata za Bombambili, Mfaranyaki, Matarawe na Mjini.

Mkomela alifafanua kuwa zoezi hilo limefanyika katika maeneo yenye mazalia ya mbu ambayo ni ya wazi yenye kuzalisha mbu wanaotaga mayai na kueneza ugonjwa wa malaria.


Kwa mujibu wa Afisa afya huyo hadi sasa jumla ya mazalia ya maji 212 na mabwawa nane yamepuliziwa dawa na kwamba zoezi hilo ni endelevu litafanyika kata hadi kata.

Amezitaja changamoto ambazo zimejitokeza hadi sasa ni kwamba utekelezaji wake umekuwa mgumu kutokana na kukosa fedha za kununua vifaa na kuwalipa wapuliziaji.

Kufuatia hali hiyo wameweza kuanza katika mitaa 49 tu iliyopo katika kata kumi kati ya mitaa 95 iliyopo katika kata 21 ndani ya Manispaa hiyo.

Changamoto nyingine ni kukosekana kwa maafisa afya katika kata nane ambao ni wataalam ambao wangeweza kusaidia katika utekelezaji wa kazi hiyo.

Pamoja na mambo mengine Afisa afya huyo anaongeza kuwa mikakati ambayo inachukuliwa ili kuweza kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni kuandaa bajeti ya upuliziaji na kuiingiza katika mpango wa utekelezaji wa mwaka 2018/2019 ili kuweza kuleta ufanisi zaidi.

Kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi la upuliziaji Manispaa ya Songea ilianza kutekeleza kazi hiyo kwa kuwashirikisha viongozi wa mitaa kwa kufanya nao mikutano elekezi wakiwemo Wenyeviti na Maafisa watendaji.

Mikutano hiyo walikuwa wakijadili masuala muhimu juu ya namna zoezi la kuua viluwiluwi vya mbu, kuhamasisha wananchi katika kutambua mazalia ya mbu na namna ya kukabiliana nayo katika maeneo yao huku wakimteua pia mpuliziaji wa viuadudu ambaye atajitolea katika kufanya kazi hiyo.


Mkomela alisema baada ya mkutano huo Wenyeviti wa mitaa na Maafisa watendaji waliweza kuteua mpuliziaji kutoka katika kila mtaa ambao walipewa mafunzo namna ya kupulizia viuadudu katika maeneo ambayo yana mazalia wazi na yale yaliyofunikwa.

No comments: