Monday, November 27, 2017

WAGANGA WAKUU MIKOA NA WILAYA WAPEWA MENO

Na Kassian Nyandindi,   
Namtumbo.

WAGANGA Wakuu wa mikoa na wilaya hapa nchini wameagizwa kuendelea kuwachukulia hatua kali baadhi ya watumishi wa sekta ya afya ambao wanajihusisha na vitendo vya wizi wa dawa za Serikali.

Kassim Majaliwa ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa agizo hilo juzi, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliojumuisha wananchi pamoja na viongozi wa wilaya ya Namtumbo katika uwanja wa michezo mjini hapa.

Alisema kuwa katika kuimarisha sekta hiyo Serikali imeongeza bajeti ya fedha kutoka shilingi bilioni 32 hadi kufikia bilioni 220 kwa mwaka huku akisisitiza dhamira ya Serikali ina lengo la kuondoa usumbufu wa upatikanaji wa dawa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zake za Serikali kote nchini.


Aliongeza kuwa baadhi ya watumishi wa afya wamekuwa chanzo cha matatizo ya upungufu wa dawa za binadamu katika sekta hiyo kutokana na tabia ya wizi ambapo alionya kwamba watumishi wa aina hiyo hawatafumbiwa macho watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Nawaagia Waganga wakuu wa mikoa na wilaya hapa nchini kuwashughulikia watumishi wote wanaojihusisha na wizi wa dawa za Serikali katika maeneo ya kutolea huduma za afya”, alisisitiza Waziri Mkuu.

Pia aliwahamasisha Madiwani kuhamasisha wananchi wao kushiriki kikamilifu katika kazi ya ufyatuaji tofali kwa ajili ya kutekeleza mpango wa ujenzi wa zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya kwa ngazi ya kata.

Alisema kuwa mpango huo ukifanikiwa wananchi watapata maeneo bora ya kutolea huduma bora za afya na Serikali itahakikisha inapeleka fedha za kutosha kwa ajili ya ununuzi wa dawa.

Pia aliwataka maafisa ugani kote nchini kuhakikisha wanatembelea wakulima mashambani ili kufahamu matatizo waliyonayo na aina ya mazao yanayostawi vizuri katika maeneo wanayoishi pamoja na kutafuta masoko ya mazao hayo yanayozalishwa katika husika badala ya kutumia muda mwingi kukaa Ofisini.

Alibainisha kuwa Serikali itaendelea kutafuta makampuni mengi zaidi kwa ajili ya kununua mazao ya wakulima ikiwemo mbaazi na korosho huku akisisitiza maafisa hao kutumia utaalam wao kuwasaidia wakulima wazingatie kanuni bora za kilimo cha kisasa ili waweze kupata mazao mengi.

No comments: