Tuesday, November 14, 2017

KUKOSEKANA SOKO LA UHAKIKA WAKULIMA SONGEA WATELEKEZA MBAAZI MASHAMBANI

Zao la Mbaazi.
Na Muhidin Amri,      
Songea.

WAKULIMA wanaojishughulisha na kilimo cha zao la mbaazi katika kata ya Mgazini Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wametelekeza zao hilo mashambani baada ya kukosa soko la uhakika.

Kata ya Mgazini ni kati ya maeneo ambayo uzalishaji mkubwa wa mazao mbalimbali unafanyika ikiwemo zao hilo.

Msimu wa mwaka huu zao hilo limekumbwa na changamoto ya kukosa soko la uhakika jambo ambalo limewafanya baadhi ya wakulima waache kuvuna mashambani walikozalisha huku wengine wakisema hawaoni sababu ya kuendelea kupoteza nguvu zao.

Katika msimu wa mwaka 2016/2017 zao la mbaazi lilikuwa linauzwa kati ya shilingi 1,000 hadi 1,500 kwa kilo lakini katika kipindi cha mwaka huu bei ya kilo moja ni kati ya shilingi 100 hadi 120 hivyo wakulima wengi wamekata tamaa na kuacha mbaazi zao mashambani bila kuvuna kutokana na kiwango hicho cha fedha kuwa kidogo na kukosa soko la uhakika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walidai kuwa hivi sasa kutokana na hali hiyo inatishia kuongezeka kiwango cha umaskini kwenye kaya zao huku baadhi yao walikuwa wakitegemea waweze kupata fedha za kupeleka watoto wao shule.

Walisema zao hilo ndilo lilikuwa zao ambalo wanategemea pia kukuza uchumi wao na kwamba wameiomba Serikali kwa kuwa haifanyi biashara hivyo iruhusu soko huria ambalo litatoa fursa kwa mkulima kwenda kutafuta soko lingine nje ya nchi.

No comments: