Tuesday, November 7, 2017

MIKOA YATAKIWA KUWEKA MAANDALIZI MAPEMA KUPOKEA WANAFUNZI KIDATO CHA KWANZA

Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo akizungumza leo na Waandishi wa habari mjini Dodoma.
Na Mwandishi wetu,

WAZIRI wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo ameitaka mikoa yote nchini, kuanza mapema maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2018 kufuatia uwepo wa ongezerko la ufaulu.

Jafo alitoa kauli hiyo leo mjini Dodoma, wakati akizungumza na Waandishi wa habari, juu ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka mwakani.

“Wakuu wa mikoa hakikisheni miundombinu iliyopo inatosha katika mikoa yenu ili watoto wote waliofaulu wapate nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza hapo Januari mwaka 2018”, alisisitiza.


Ameitaja mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Kagera, Njombe, Tanga, Morogoro, Lindi, Rukwa, Pwani, Mtwara na Songwe kuwa ndiyo yenye idadi kubwa na kwamba maandalizi ya madarasa, vyoo na madawati yatahitajika kwa kiwango kikubwa.

Kadhalika amewataka Makatibu tawala wa mikoa, kusimamia zoezi la uchaguzi wa wanafunzi tarajiwa wa kidato cha kwanza ili ifikapo Disemba 8 mwaka huu wawe wamekwisha tangaza.

Pia Jafo ameagiza kufanyika uchambuzi ili kubaini sababu zilizopelekea watahiniwa zaidi ya asilimia moja kutofanya mitihani katika mikoa ya Geita, Katavi, Mara, Rukwa, Songwe, Dodoma na Manyara kwa lengo la kuondoa mdondoko wa wanafunzi kutoka ngazi moja hadi nyingine.

Vilevile amezitaka halmashauri zilizopata ufaulu chini ya asilimia hamsini kujiwekea mikakati ya kupandisha ufaulu wa wanafunzi, ambapo halmashauri hizo ni pamoja na Mkalama, Meatu na Simanjiro.

Matokeo ya darasa la saba yalitangazwa rasmi hivi karibuni ambapo jumla ya watahiniwa wapatao 662,035 walifaulu kwa kupata daraja A, B na C, ikiwa ni sawa na asilimia 72.76 ya watahiniwa wote.


Ofisi ya Rais TAMISEMI ndiyo yenye dhamana na usimamizi wa elimu ya awali, msingi na sekondari imechukua hatua za makusudi, kupunguza au kuondoa wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba kutopangiwa shule na kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.

No comments: