Saturday, November 18, 2017

AGIZO LA RAIS MAGUFULI LA PUUZWA

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

WAKATI Rais Dokta John Pombe Magufuli akisisitiza suala la usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali hapa nchini, hali hiyo imekuwa kinyume kwa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, ambapo agizo hilo linaonesha kupuuzwa kutotekelezwa ipasavyo na sasa mji huo umeshamiri uchafu katika mitaa yake na kuwa kero katika jamii.

Mara baada ya Rais Dokta Magufuli kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana alianzisha Operesheni maalum ya kufanya usafi ambayo imeendelea hadi sasa, kwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa ndiyo siku ya usafi kuanzia alfajiri hadi saa 5:00 asubuhi.

Katika uzinduzi huo Rais alifanya usafi eneo la Feri jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu walifanya eneo la Kariakoo huku viongozi wengine wakishirikiana na wananchi kufanya usafi katika maeneo yao.

Hivyo basi pamoja na wananchi wa mji huo kuchangishwa fedha mara kwa mara kwa ajili ya kufanyia utekelezaji wa kazi hiyo lakini hakuna jitihada zinazo onesha kuzaa matunda.


Kufuatia hali hiyo, baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo ambalo limeketi hivi karibuni mjini hapa, limelalamikia uongozi husika kwa kutochukua hatua za makusudi katika kuhamasisha jamii ili iweze kushiriki kikamilifu kuondoa taka kwenye maeneo hayo.

Vilevila baraza hilo limeutaka uongozi huo kuchukua hatua za haraka kuondoa taka zilizofurika kwenye maghuba yaliyopo mjini hapa kwani imefikia hatua baadhi ya maghuba kutoa harufu kali na kuhatarisha usalama wa afya za wananchi.

Grace Millinga ambaye ni diwani wa viti maalum kata ya Mbinga mjini, alisema kuwa tatizo kubwa lipo kwa wataalamu husika ambao wanasimamia utekelezaji wa jambo hilo ambapo hata madiwani hawajui ni namna gani walivyopanga mkakati wa namna ya kuzoa taka hizo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti tunataka leo hii watueleze hapa katika kikao hiki, wamejipangaje namna ya kuzoa zile taka kwenye maghuba huu mji wetu ni mchafu”, alisema Millinga.

Naye diwani wa Mbinga mjini A, Aurelia Ntani akizungumzia juu ya tatizo hilo ambalo limefikia hatua ya kuwa kero kwa jamii aliongeza kuwa hata ghuba lililokuwa eneo la Soko kuu mjini hapa, ambako vyakula vingi vimekuwa vikiuzwa hapo taka nyingi zimerundikana zikitoa harufu kali huku inzi wakiwa wamezagaa na hakuna usafi unaofanyika.

Kwa upande wake baraza hilo la Madiwani wa mji wa Mbinga lilipomtaka Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji huo, Robert Kadaso Mageni kutolea maelezo juu ya kero hiyo alikiri hali ya mji kuwa mchafu na kueleza kuwa kuna mikakati ambayo inaendelea kufanyika katika kupambana na hali hiyo.

“Suala la usafi hapa mjini ni kweli maghuba ni machafu tumeshauri kuna vikundi vitakavyokuwa vinajishughulisha na masuala ya usafi katika mji vitajipanga ili kuweza kuanza kutatua kero hii,

“Tunataka kwa wale ambao ni wazalishaji wa taka, wazitunze taka wao wenyewe na halmashauri itakuwa inazipitia na kwenda kuzimwaga katika eneo husika kwa ajili ya kuziteketeza”, alisema Mageni.

Mageni alisema kuwa kwa kushirikiana na watendaji waliopo katika kata husika utekelezaji huo utakuwa unafanyika lakini pia kuna sheria mpya ambazo zinaandaliwa na sasa wamefikia hatua ya mwisho ya kumaliza taratibu husika ili ziweze kuanza kufanya kazi ya kusimamia na kudhibiti kero hiyo.

No comments: