Thursday, November 16, 2017

KOREA KUSINI NA TANZANIA KUIMARISHA USHIRIKIANO KITUO CHA ELIMU KUJENGWA MBINGA

Uzinduzi wa ujenzi Kituo cha elimu ulifanyika jana katika kitongoji cha Lulambo kata ya Matarawe mjini hapa, ambapo Balozi wa Korea kusini Song, Geum - Young ndiye aliyeshiriki kufanya kazi hiyo ya uzinduzi kwa kushirikiana na viongozi wa wilaya ya Mbinga.  
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa ushirikiano uliopo kati ya Korea kusini na Tanzania, utaendelea kuimarishwa katika kusaidia kukuza maendeleo ya wananchi hapa nchini, hususan katika kuboresha sekta ya elimu na afya.

Aidha wananchi wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wameombwa kuzingatia hilo ili viongozi wa ubalozi wa Korea kusini waweze kufanikiwa hatua ya kuboresha sekta hizo wilayani humo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Song, Geum – Young ambaye ni Balozi wa nchi hiyo hapa Tanzania alisema hayo jana wakati alipokuwa kwenye sherehe ya uzinduzi wa shughuli ya ujenzi wa Kituo cha elimu zilizofanyika katika mtaa wa Lulambo kata ya Matarawe mjini hapa.

“Ushirikiano wetu tulionao tutaendelea kusaidia Watanzania na wanambinga kwa ujumla, lakini pia tutahakikisha Korea kusini na Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye urafiki mzuri”, alisema Song, Geum – Young.

Balozi huyo aliongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho ambacho kitakuwa chuo cha mafunzo ya sekta ya elimu na afya kutaweza kuinufaisha pia jamii ya kutoka maeneo mbalimbali nje ya wilaya hiyo.

Alifafanua kuwa ujenzi huo utaanza mapema kuanzia sasa na kwamba utagharimu dola za Kimarekani milioni 150.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye naye akizungumza katika sherehe hizo za uzinduzi aliushukuru Ubalozi huo wa Korea kusini kwa moyo walionao katika kushirikiana na wanambinga kuleta maendeleo hayo.

“Mimi kwa niaba ya wananchi wangu nichukue nafasi hii kuwakaribisha nasema karibuni sana, Ofisi yangu itatoa ushirikiano mkubwa kwenu kwa jambo lolote mtakalohitaji kupata ushirikiano kutoka kwangu”, alisema.

Nshenye alieleza kuwa huduma zitakazotolewa hapo wananchi wa wilaya hiyo wanapaswa kuzipokea kwa mikono miwili kwani wataweza kupata fursa ya kuweza kukuza ajira na kujenga mahusiano mazuri kati yao na wananchi wa Korea kusini.

Pia alisisitiza kuwa eneo hilo ambalo ujenzi unafanyika lisiingiliwe ovyo na wananchi badala yake waendelee kutoa ushirikiano kwa shughuli zitakazofanyika hapo kwa faida ya wananchi wote.

No comments: