Thursday, November 9, 2017

CHRISTINE MNDEME AWAPA SOMO MADIWANI MBINGA AWATAKA KUSIMAMIA MIRADI YA WANANCHI

Na Mwandishi wetu,     
Mbinga.

MADIWANI waliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamesisitizwa wahakikishe kwamba wanasimamia ipasavyo maendeleo ya wananchi ili mwisho wa siku wananchi waliowachagua waendelee kuwa na imani nao.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa mkoa huo, Christine Mndeme wakati alipokuwa juzi katika ziara yake ya kikazi wilayani hapa huku akiwataka Madiwani hao katika kata zao kufanya mikutano na wananchi ambayo inalenga kujadili masuala ya kimaendeleo.

“Ndugu zangu maana mkizembea kufanya hivi siku ya mwisho wa utawala wenu kule katani waliotuajiri hawatatuelewa tena”, alisema Mndeme.


Vilevile aliwataka kuwa na mahusiano mazuri kati yao na watendaji wa halmashauri lakini pale wanapoona mambo ya kimaendeleo hayaendi vizuri wanapaswa kuchukua hatua haraka kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa.

Kwa upande wa kukuza uchumi alisisitiza ufanyike uhamasishaji wa kutafuta wawekezaji waliopo ndani na nje ya wilaya, kwa kuwapatia fursa ya kujenga viwanda ambavyo vitasaidia kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa na hatimaye wananchi waweze kuondokana na umaskini.

“Tunapokuwa na viwanda vya usindikaji tutaweza kukuza uchumi wa wilaya yetu, tuitangaze Mbinga ili watu waje wawekeze hapa tusiweke urasimu”, alisema.

Mndeme amewataka pia Wakurugenzi watendaji waliopo kwenye halmashauri hizo waondoe urasimu pale wawekezaji hao wanapojitokeza na kutaka kuwekeza kwa namna mbalimbali ikiwemo ujenzi huo wa viwanda.

Akizungumza mara baada ya Mndeme kutoa nasaha zake naye Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Ambrose Nchimbi alisema kuwa watazingatia maagizo na maelekezo aliyoyatoa Mkuu huyo wa mkoa ili kuweza kufikia malengo husika kwa manufaa ya wananchi.


Nchimbi alimuomba pia Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma atatue tatizo la upungufu wa walimu kwa shule za msingi na sekondari ambalo linaikabili wilaya ya Mbinga kwa muda mrefu na ndiyo kikwazo kikubwa kinachoifanya wilaya ishindwe kusonga mbele katika sekta ya elimu ambapo naye alisema atalifanyia kazi ili kuweza kuondokana na hali hiyo.

No comments: