Sunday, November 19, 2017

UUZWAJI MAGUNIA KIHOLELA MTWARA WAMTIBUA NAIBU WAZIRI KILIMO

Naibu Waziri wa Kilimo, Mary Machuche Mwanjelwa akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Gasper Byakwana wakikagua baadhi ya magunia ambayo yamewasilishwa katika Ofisi ndogo ya Chama cha ushirika wilayani Masasi mara baada ya kumalizika mnada wa tano wa Korosho kijijini Chiungutwa wilayani humo. 
Na Mathias Canal,
Mtwara.

NAIBU Waziri wa kilimo, Mary Machuche Mwanjelwa amemtaka Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani Mtwara, kukamilisha haraka kazi ya uchunguzi kwenye bodi za vyama vya ushirika mkoani humo ili kubaini sababu zilizosababisha kuuzwa kwa magunia kiholela bila kufuata taratibu.

Alisema kuwa kumalizika kwa uchunguzi huo kutarahisisha kuchukuliwa haraka hatua kali za kisheria kwa wale wote watakaobainika kukiuka sheria namba 17 ya vyama vya ushirika.

Naibu Waziri huyo alitoa agizo hilo wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji na kata ya Chiungutwa, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara mara baada ya kugundua kuwa kuna viashiria vya ukiukwaji wa taratibu katika upatikanaji wa magunia ya kuhifadhia korosho wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapa.

Sambamba na hilo Mwanjelwa wakati wote alipokuwa kwenye mkutano huo ameshuhudia malalamiko kutoka kwa wakulima wa zao la Korosho wa Chama cha Ushirika cha Masasi-Mtwara Cooperative Union Limited (MAMCU) kuhusu ucheleweshwaji wa upatikanaji wa magunia hayo kutoka kwa mzabuni, mapungufu ya kilo kati ya PDA na WHRs ghala kuu, ikiwa ni pamoja na kuchelewa kwa malipo ya wakulima kwa njia ya benki kutoka kwa wanunuzi.

Katika ziara yake hiyo kilio cha wananchi wengi na wakulima walisisitiza zaidi kuhusu kukosekana kwa magunia hayo huku wakieleza kuwa wakati mwingine kuchelewa kufika au kutowafikia kabisa jambo ambalo linachangia kupunguza thamani ya zao la korosho.

“Nataka Mrajisi ufanye na ukamilishe kazi yako ya uchunguzi haraka na baada ya kuipata taarifa hiyo hatua stahiki zitachukuliwa kwa wale wote watakaogundulika kukiuka sheria za nchi”, alisema Mwanjelwa.

Mbali na agizo hilo Naibu Waziri huyo wa Kilimo pamoja na Wabunge wa Mkoa huo walipata nafasi ya kujionea mnada wa tano wa ununuzi wa zao la Korosho unavyoendelea.

Hata hivyo mnada wa tano ulishuhudiwa Kilogramu 7,524,104 za Korosho zikiuzwa kwa thamani ya zaidi ya Bilioni 30.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanjelwa alisema kuwa Wizara yake itayafanyia kazi haraka mapendekezo ya tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa huo, Gelasius Gasper Byakanwa kufanya uchunguzi kuhusu mwenendo mzima wa magunia hayo pamoja na upatikanaji wake.

No comments: