Thursday, November 16, 2017

KLINIKI TIBA MBADALA SONGEA ZAFUNGIWA KUTOA HUDUMA

Hiki ni moja kati ya kituo cha tiba mbadala kilichopo mjini Songea ambacho kimefungwa kisitoe huduma kutokana na kutokidhi vigezo husika.
Na Albano Midelo,    
Songea.

ZIARA ya kushitukiza ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mganga mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Gozibert Mutahyabarwa imefanyika katika Kliniki zilizopo katika Manispaa ya Songea na kubaini Kliniki mbili zinaendeshwa kinyume cha taratibu na sheria za tiba asili na tiba mbadala.

Baada ya ukaguzi huo kufanyika na timu mbili za wataalam wa afya ngazi ya mkoa huo na wale wa Manispaa hiyo wameweza kubaini vituo vya Ndulu Herbal Clinic kilichopo Mahenge na Bethlehemu Samaritan Clinic kilichopo Mfaranyaki Songea vinapima wagonjwa kwa kutumia kipimo cha Qantum Resonance Magnetic Analzer ambacho kimepigwa marufuku na Serikali.

Mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Gozibert alisema vituo vyote vya tiba asili viliandikiwa barua kutoka Manispaa ya Songea kuacha kutumia kipimo hicho, ambacho kinawarubuni wananchi kuwa wanaumwa magonjwa mengi wakati sivyo ndivyo hivyo kuwafanya walipe gharama kubwa kwa ajili ya matibabu ambazo ni kati ya shilingi 150,000 hadi 300,000.


Vituo hivyo vimekaidi na kuendelea kutumia kipimo hicho kupima wagonjwa ambapo utafiti uliofanywa na madaktari ulibaini kipimo hicho kinatoa vipimo vya uongo na hakina viwango vyenye ubora.

Licha ya kutumia kipimo hicho ambacho kimepigwa marufuku, mapungufu mengine ambayo yamebainika katika operesheni hiyo ni pamoja na vituo hivyo kutumia watalaamu ambao hawana sifa ya kuwa madaktari na wahudumu wa afya ambapo kituo cha Bethlehemu Samaritan Clinic pia hakijasajiliwa.

Kutokana na mapungufu hayo vituo hivyo vimefungwa kuanzia Novemba 10 mwaka huu na mashine walizokuwa wanazitumia zimechukuliwa na idara ya afya Manispaa ya Songea.

Vituo hivyo vinaweza kufunguliwa iwapo vitafanya marekebisho maagizo ya Serikali na kukidhi vigezo husika vya Wizara ya afya kwa kuzingatia taratibu, sheria, kanuni na miongozo husika ili viweze kuendelea kutoa huduma rafiki na salama kwa watumiaji.

Dokta Gozibert alisisitiza kuwa kutokana na ukubwa wa tatizo hilo ziara ya kushitukiza zitafanyika katika mkoa mzima wa Ruvuma ili kulinda maisha ya wananchi kutokana na matumizi yasiyokuwa salama katika tiba asili na tiba mbadala.

No comments: