Tuesday, November 14, 2017

CHANGAMOTO YA MAGUNIA ADUI WA MAENDELEO KIWANDA CHA KUKOBOA KAHAWA MBINGA

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

KAMPUNI ya Kiwanda cha Kukoboa Kahawa Wilayani Mbinga (MCCCO) mkoa wa Ruvuma, inalazimika kuwatumia wazabuni waliopo nje ya nchi kusambaza magunia ya kuhifadhia kahawa safi ambayo inakobolewa kiwandani hapo, kutokana na mzabuni aliyepewa kazi hiyo hapa nchini kushindwa kufanya kazi hiyo.

Aidha kufuatia hali hiyo, Serikali imeombwa kuruhusu wazalishaji wa magunia hayo wawe wengi ili kuweza kunusuru hali hiyo na kufanya kahawa inayokobolewa hivi sasa kiwandani hapo iweze kuhifadhiwa katika mazingira mazuri.

Injinia Rabiel Ulomi ambaye ni Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho, alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza ofisini kwake na mwandishi wa habari hizi juu ya maendeleo ya uzalishaji wa zao la kahawa wilayani humo.

Ulomi alifafanua kuwa kazi ya usambazaji wa magunia hayo ilikuwa ikifanywa na kampuni ya Mohamed Enterprises kutoka jijini Dar es salaam, kwa miaka mingi lakini hawajui kwa nini mzabuni huyo aliyepewa dhamana hiyo amesitisha huduma ghafla ya kutosambaza magunia hayo.

“kuhusu changamoto hii ya uhaba wa magunia ni kweli tunayo, hili tatizo limejitokeza kwa ukubwa hasa kwa mwaka huu kwa sababu mzalishaji mkubwa wa magunia tunayemtegemea hapa kwetu ni Mohamed Enterprises kutoendelea kutoa huduma na hatujui kwa nini amesitisha licha ya uongozi wetu kuwasiliana na bodi ya kahawa”, alisema Ulomi.

Alifafanua kuwa magunia wanayotumia sasa inawalazimu kuagiza kutoka India na kwamba tatizo hilo wakati mwingine limekuwa linakwamisha hali ya uhifadhi wa kahawa katika mazingira bora.

“Tunafikiri kwamba kwa sera za Tanzania ya viwanda ni jambo ambalo linapaswa kuangaliwa sana na kufanyiwa utekelezaji ili kuweza kuachana na mfumo huu wa kuagiza malighafi nje ya nchi”, alisisitiza.

Pamoja na mambo mengine Meneja huyo wa uzalishaji kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga, aliwataka pia wadau wa kahawa wilayani hapa kujitokeza kwa wingi na kujenga maghala ya kuhifadhia zao hilo ili kuweza kuondokana na tatizo la upungufu wa maghala ambalo linaikabili wilaya hiyo.

No comments: