Wednesday, November 22, 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA KUFANYA ZIARA KESHO MKOANI RUVUMA

Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kesho Novemba 23 mwaka huu anatarajia kuwasili mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya siku tatu na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa dini, vyama vya siasa na Serikali katika uwanja wa ndege uliopo Ruhuwiko mjini Songea.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mkuu wa Mkoa huo, Christine Mndeme akizungumza leo na vyombo mbalimbali vya habari Ofisini kwake alisema kuwa Waziri Mkuu huyo anatarajia kuwasili katika uwanja huo mjini hapa majira ya saa saba kamili mchana.

Alisema kuwa mara baada ya kuwasili atapokea taarifa ya maendeleo ya mkoa huo na ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uwanja wa ndege mjini Songea na baada ya hapo ataelekea wilayani Namtumbo ambapo atafungua ghala la MIVARF, kuongea na madiwani, watumishi wa umma na wananchi wa wilaya hiyo katika mkutano wa hadhara.


Mndeme alifafanua kuwa atakapokuwa wilayani humo, Novemba 24 mwaka huu Majaliwa ataendelea na ziara yake atasalimiana na wananchi wa kijiji cha Mchomoro na kisha kuelekea wilayani Tunduru ambapo atafanya mkutano wa hadhara, kijiji cha Rahaleo na kusalimiana na wananchi wa kijiji cha Milonde kisha kuelekea Tunduru mjini.

Atakapokuwa wilayani Tunduru atatembelea kituo cha afya Nakayaya, ghala la kuhifadhia korosho na kupokea taarifa ya Chama kikuu cha ushirika (TAMCU) na kuzungumza na wananchi wa wilaya hiyo katika uwanja wa michezo wilayani humo.

Mkuu huyo wa mkoa amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye maeneo yote ambayo Waziri Mkuu atapita pamoja na kuhutubia mikutano ya hadhara, ili waweze kupata fursa nzuri ya kumsikiliza na kupokea maelekezo atakayotoa hususan katika shughuli za utekelezaji wa maendeleo ya wananchi.

No comments: