Wednesday, November 8, 2017

UJENZI KITUO CHA AFYA KALEMBO UKAMILIKE KWA WAKATI ULIOPANGWA

Christine Mndeme ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma akizungumza na wananchi wa kata ya Kihungu katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo, wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ambapo aliwataka washiriki kikamilifu katika shughuli ya ujenzi wa kituo cha afya Kalembo kilichopo katika kata hiyo ili ujenzi wake uweze kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christine Mndeme akishiriki juzi katika shughuli za ujenzi wa kituo cha afya Kalembo kilichopo katika kata ya Kihungu Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ambapo ujenzi wa kituo hicho unagharimu shilingi milioni 500.
Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

AGIZO limetolewa kuwa fisadi au mwizi yeyote atakayejitokeza kuiba sehemu ya fedha shilingi milioni 500 ambazo zimetolewa na Serikali, kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kalembo kilichopo katika kata ya Kihungu Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, haraka achukuliwe hatua za kisheria asionewe huruma.

Mkuu wa Mkoa huo, Christine Mndeme alitoa agizo hilo juzi akimtaka Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha hizo ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa, wakati alipokuwa ametembelea eneo la ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa lengo la kujionea ujenzi ambao unaendelea kufanyika huko.

Alisema kuwa fedha hizo ambazo zimetolewa na Serikali ya awamu ya tano zinalenga kuboresha huduma ya afya katika kata hiyo ili wananchi wanaoishi huko waweze kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa kilometa 35 kwenda hospitali ya wilaya kutafuta matibabu pale wanapougua.


Mndeme alifafanua kuwa ushirikiano katika kukamilisha kazi hiyo kati ya wananchi na viongozi wanaosimamia ujenzi huo ni muhimu uzingatiwe ili ujenzi wa majengo husika uweze kukamilika kwa wakati uliopangwa.

“Hizi fedha ni za Watanzania, Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Magufuli katuletea hapa tuweze kuboresha mazingira ya kutolea huduma ya afya na hatimaye wanambinga waweze kunufaika na matunda ya Serikali yao ya wamu ya tano”, alisema Mndeme.

Akizungumza na wananchi wa kata hiyo ya Kihungu aliwataka pia kutovamia eneo la ujenzi wa kituo hicho ikiwemo pasitokee wizi wa vifaa vya ujenzi ambavyo vimenunuliwa na kuletwa hapo kwa ajili ya kukamilisha shughuli za ujenzi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Nshenye alimhakikishia Mkuu wa mkoa huyo kwamba atasimamia ipasavyo maelekezo yote yanayopaswa kutekelezwa katika shughuli za ujenzi wa kituo cha afya Kalembo ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.

Hata hivyo ujenzi huo unatekelezwa kwa kujenga jengo la upasuaji, maabara, nyumba ya mganga, jengo la kuhifadhia maiti, wodi ya akina mama na watoto na kwamba ujenzi wake unapaswa kukamilika ifikapo Disemba 30 mwaka huu.
 

No comments: