Tuesday, November 14, 2017

WANANCHI MWENGEMSHINDO SONGEA KULIPWA FIDIA

Meya wa Manispaa Songea, Abdul Hassan Mshaweji akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika hivi karibuni mjini hapa, juu ya mikakati ya Serikali katika kuwaletea maendeleo ya wananchi.
Na Albano Midelo,   
Songea.

IMEELEZWA kuwa Serikali hapa nchini, imekubali kuwalipa fidia ya ardhi shilingi bilioni 3.3 wananchi wanaoishi katika kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Aidha eneo ambalo hulipwa fidia ni lile lenye ukubwa wa ekari 5,000 lililochukuliwa na Serikali katika mwaka wa fedha wa 2008/2009 kwa ajili ya eneo maalum la Ukanda wa Uwekezaji Viwanda (EPZA).

Hayo yalisemwa na Meya wa Manispaa hiyo, Abdul Hassan Mshaweji wakati alipokuwa akitoa taarifa katika mkutano wa baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Songea lililoketi mjini hapa.


Mshaweji aliliambia baraza hilo kuwa Kamati maalum ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mbunge wa Songea mjini, Leonidas Gama ilifanikiwa kwenda Dodoma kukutana na uongozi husika na hatimaye kuweza kufikia muafaka wa kulipa fidia hiyo.

Alifafanua kuwa Serikali katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 italipa fidia ya shilingi bilioni 1.5 kwa wananchi hao ili kupunguza deni hilo ambalo wananchi wamekuwa wakidai kwa muda mrefu.

Wananchi 1,181 wa kata ya Mwengemshindo wanadai fidia ya shilingi bilioni 3.3 ambapo hadi sasa Serikali imelipa shilingi bilioni mbili za fidia kwa wananchi hao.

Wakichangia taarifa hiyo baadhi ya madiwani wameiomba Serikali kulipa fidia hiyo haraka kwa kuwa wananchi wamechoka kusubiri ambapo baadhi yao wamefariki dunia bila kupata haki yao. 

Diwani wa kata ya Mwengemshindo, Osmundi Kapinga alisema Serikali ilichukua ekari 5,000 za wananchi miaka kumi iliyopita ambapo hadi sasa fedha za fidia ambazo zimelipwa ni shilingi bilioni mbili tu kati ya fedha zaidi ya shilingi bilioni tano ambazo wanadai wananchi hao.

“Katika mkutano mkuu wa kata uliofanyika hivi karibuni tumeazimia kuchukua ardhi yetu bila masharti yoyote ili tuweze kuzalisha na kujenga nyumba kwa sababu wananchi wamekata tamaa na kuchoshwa na ahadi ambazo hazitekelezeki kwa muda mrefu sasa”, alisema Kapinga.

Naye Naibu Meya wa Manispaa ya Songea, Yobo Mapunda alikiri kuwa madai hayo ni ya muda mrefu ndiyo maana wananchi wamekata tamaa, hata hivyo alisema anaimani na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ni sikivu na itaweza kulipa kabla ya mwaka huu wa fedha haujakwisha.

No comments: