Monday, November 20, 2017

DIWANI MBINGA MJINI B AMSHUKURU MBUNGE SIXTUS MAPUNDA KWA KUUNGA MKONO UJENZI WA VYOO VYA WANAFUNZI SHULE YA MSINGI MBINGA

Katibu wa Mbunge wa jimbo la Mbinga mjini, Geddy Ndimbo akiwa ameshikana mkono na walimu wa shule ya msingi Mbinga mara baada ya kukabidhi vifaa vya ujenzi wa choo cha wanafunzi wa shule hiyo ambavyo vilitolewa na Ofisi ya Mbunge wa jimbo hilo Sixtus Mapunda, upande wa kulia aliyevaa koti rangi nyeusi ni diwani wa kata hiyo, Frank Mgeni ambaye naye alishiriki wakati wa makabidhiano hayo.


Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

OFISI ya Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, imetoa vifaa vya ujenzi kwa shule ya msingi Mbinga vyenye thamani ya shilingi milioni 1,178,000 kwa ajili ya kukamilisha kazi ya ujenzi wa choo cha wanafunzi wa shule hiyo.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Mbunge wa jimbo hilo Sixtus Mapunda Katibu wa Mbunge huyo, Geddy Ndimbo alisema kuwa vifaa walivyokabidhi wanaunga mkono nguvu za wananchi ambao walijitolea kujenga vyoo vya matundu nane ili wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo waweze kuwa na mazingira mazuri yenye vyoo vya kisasa.

Ndimbo alifafanua kuwa shule hiyo ambayo ipo katika kata ya Mbinga mjini B vyoo walivyokuwa wanatumia watoto hao hapo awali, vilikuwa chakavu havifai kwa matumizi hivyo anawapongeza wananchi waliojitokeza na kuchangia michango yao ya ujenzi huo.


Vifaa vya ujenzi walivyokabidhi ni saruji mifuko 25, masinki nane ya vyoo, mabomba manne ya kutolea uchafu na viungo vyake (T – Joint).

Pia aliongeza kuwa Ofisi ya Mbunge huyo inachimba kisima cha maji shuleni hapo ambacho baadaye watajenga pampu itakayokuwa inatoa maji kwa ajili ya matumizi ya watoto hao na walimu.

Vilevile katika kata hiyo ambayo ina shule ya Sekondari Mbinga alisema kuwa watakabidhi tenki kubwa la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 2,000 ambalo lina thamani ya shilingi 700,000 ili kuwawezesha wanafunzi na walimu wanaosoma katika shule hiyo waweze kuhifadhi maji safi na salama kwa ajili ya matumizi yao mbalimbali.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Mbinga mjini B, Frank Mgeni amenukuliwa akitoa shukrani zake akisema, “kwa nafasi ya pekee nimshukuru sana Mbunge wangu Sixtus na Katibu wake Geddy kwa kuniunga mkono katika ujenzi wa choo hiki toka kinaanza kujengwa hadi leo napokea tena vifaa vingine ambapo baada ya wiki mbili choo kitaanza kutumika,

“Niseme tu vifaa vyote vya kiwandani vya ujenzi wa choo hiki vimetoka kwa Mbunge pekee natambua tena mchango wake wa fedha kwa ajili ya kuchimba kisima cha maji shuleni hapa”.

No comments: