Monday, November 20, 2017

KAMBAS GROUP OF COMPANIES YATOA MSAADA VIFAA VYA UJENZI SHULE YA MSINGI MIPETA SONGEA

Mkurugenzi wa kampuni ya Kambas Group of Companies, Yahaya Yusuph wa pili kushoto akikabidhi msaada wa bati 100 kwa Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema juzi kwa ajili ya ukarabati wa vyumba vinne vya madarasa, Ofisi mbili za walimu na nyumba mbili za walimu wa shule ya msingi Mipeta kata ya Muhukuru Halmashauri ya wilaya ya Songea ambayo paa zake ziliezuliwa na upepo ulioambatana na mvua mapema mwanzoni mwa mwezi huu.

Mkurugenzi wa kampuni ya Kambas Group of Companies, Yahaya Yusuph katikati akikabidhi msaada wa mifuko ya saruji kwa Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema kwa ajili ya ukarabati wa shule ya msingi Mipeta na nyumba mbili za walimu kata ya Muhukuru halmashauri ya wilaya ya Songea.
Na Muhidin Amri,     
Songea.

KAMPUNI ya Kambas Group of Companies, inayofanya utafiti wa makaa ya mawe katika kitongoji cha Mipeta na Manyamba kata ya Muhukuru Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, imetoa msaada wa mifuko ya saruji 150 na bati 100 kwa ajili ya ukarabati wa vyumba vinne vya madarasa, nyumba mbili za walimu na ofisi ya shule ya msingi Mipeta iliyopo wilayani humo.

Mwanzoni mwa mwezi huu upepo mkali ulioambatana na mvua uliezua paa katika baadhi ya madarasa, ofisi za walimu pamoja na nyumba mbili za walimu hali iliyosababisha wanafunzi kuanzia darasa la kwa kwanza hadi sita kulazimika kusomea vyumba viwili vya madarasa huku walimu walioezuliwa nyumba zao za kuishi wakiomba hifadhi ya kulala kwa walimu wenzao na wenyeji wa kitongoji hicho.

Akikabidhi msaada huo jana kwa Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Yahaya Yusuph alisema wameamua kutoa vifaa hivyo vya ujenzi ikiwa ni mkakati wa kampuni yake kuunga mkono mpango wa Serikali ya Rais Dokta John Pombe Magufuli ya kutoa elimu bure, hivyo yeye kama mdau wa maendeleo ameona ni vyema kuchangia vifaa hivyo ili watoto hao waweze kuendelea na masomo katika mazingira mazuri.

Alisema kuwa msaada huo alioutoa una thamani ya shilingi milioni 5.5 ambazo zitawezesha kurudisha miundombinu ya shule hiyo kama ilivyokuwa hapo awali ili walimu na wanafunzi waweze kuondokana na adha hiyo wanayoipata sasa.

Alisema kuwa baada ya kuona tatizo hilo kupitia kituo kimoja cha Televisheni aliguswa na kuamua kutoa msaada huo wa mabati na saruji vyote vikiwa na thamani hiyo kwa lengo la kuweza kupunguza madhara hayo yaliyojitokeza.

Kadhalika ameyataka makampuni mengine ndani na nje ya nchi na wale watu wenye uwezo kujitokeza kuisaidia shule hiyo vifaa na mahitaji mengine, na sio kuiachia Serikali peke yake ambayo inakabiliwa na majukumu mengi ya utekelezaji wa maendeleo ya wananchi.

Akipokea msaada huo mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema mbali na kuishukuru kampuni hiyo kwa msaada wake alisema kuwa upepo huo ambao uliambatana na mvua ulisababisha madhara makubwa  hata kwa wananchi ambapo nyumba 29 ziliezuliwa na nyingine kuta zake kuanguka.

Mgema aliongeza kuwa mahitaji halisi kwa madhara yaliyotokea katika tukio hilo ni bati 330 na saruji mifuko 380 hata hivyo kampuni hiyo imetoa nusu ya sehemu ya mahitaji yao ambapo ametoa wito kwa watu mbalimbali kuangalia uwezekano wa kusaidia vifaa vingine vitavyoweza kusaidia kurudisha miundombinu ya shule hiyo katika hali yake ya kawaida kama ilivyokuwa hapo awali.

No comments: