Monday, October 30, 2017

KIPINDUPINDU CHAINGIA DODOMA MTU MMOJA AFARIKI DUNIA

Ummy Mwalimu Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto.

Na Mwandishi wetu,
Dodoma.

MTU mmoja amefariki dunia na wengine nane kuugua ugonjwa wa kipindupindu mkoani Dodoma, ambapo inadaiwa kuwa ugonjwa huo uliwapata wakiwa kwenye sherehe ya harusi iliyofanyika katika kijiji cha Mlowa barabarani wilayani Chamwino.

Dokta Charles Kiologwe ambaye ni Mganga mkuu wa Mkoa wa Dodoma alisema kuwa ugonjwa huo uliingia mkoani humo Oktoba 19 mwaka huu huku akizitaja wilaya zilizokumbwa na ugonjwa kuwa ni Bahi, Chamwino na Kongwa.

Alisema ugonjwa wa kipindupindu umeingia katika mkoa wa Dodoma ambapo baadhi ya watu wameugua na mmoja amepoteza maisha wilayani Bahi.


Dokta Kiologwe alisema ugonjwa huo uliibuka kwenye sherehe hizo ambako kulikuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo na kwamba baada ya sherehe hizo kumalizika, siku ya pili watu wawili wa familia moja waligundulika kuugua ugonjwa huo.

Alisema kuwa timu ya madaktari wa mkoa kwa kushirikiana na wa wilaya ya Chamwino walifungua kambi ya muda ili kuweza kuzuia hali hiyo isiweze kuenea.

“Baada ya kudhibiti ugonjwa huu kwenye wilaya ya Chamwino tulipata taarifa ya mgonjwa mwingine ambaye alikuwapo kwenye sherehe hiyo ambaye ni mkazi wa Chibelela wilayani Bahi kuwa anaugua ugonjwa huu tumeweza kuchukua hatua na kudhibiti hali hii”, alisema Dokta Kiologwe.

Alibainisha kuwa mume wa mgonjwa huyo wakati akimuuguza mke wake huyo hakujua kama ana ugonjwa wa kipindupindu kwa kuwa alikuwa akimuuguza kienyeji na matokeo yake na yeye akakumbwa na kipindupindu na kumsababishia kifo.

Vilevile alisema wagonjwa wengine wawili waliokuwa safarini wakitokea kijiji cha Mlowa barabarani waliugua ugonjwa huo na kulazimika kulazwa katika Kijiji cha Nkurabi ili kupatiwa matibabu.

Dokta Kiologwe alieleza kuwa mpaka sasa watu tisa wameugua ugonjwa huo na kati yao mmoja amefariki na tayari hatua zimechukuliwa kwa kufungua kambi za muda kijiji cha Mlowa barabarani (Chamwino), Chibelela (Bahi), Nkurabi (Manispaa ya Dodoma) na Kongwa.

Alitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari za ugonjwa huo kwa kufanya usafi na kuzingatia kanuni za afya katika maeneo yao wanayoishi ili kuweza kujiepusha na kukumbwa na ugonjwa huo. 

No comments: