Saturday, October 7, 2017

MANISPAA SONGEA YAFAULISHA KIDATO CHA SITA KWA ASILIMIA 97

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Hassan Mshaweji.
Na Albano Midelo,
Songea. 

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imeendelea kufanya vizuri katika mtihani wa Taifa kidato cha sita, baada ya kufaulisha kwa asilimia 97.2.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, shule tano za Serikali kidato cha sita wanafunzi ambao walipata daraja la kwanza ni 62 na kwamba kati yao wavulana ni 34 na wasichana ni 28.

Daraja la pili lina jumla ya wanafunzi 471 kati yao wavulana ni 174 na wasichana 297 ambapo daraja la tatu wapo jumla ya wanafunzi 507 kati yao wavulana ni 179 na wasichana 328.


Kulingana na matokeo hayo, daraja la nne lina wanafunzi 47 kati yao wavulana 23 na wasichana 24 na wale waliopata daraja sifuri ni 24 kati yao wavulana 10 na wasichana14.

Shule za serikali ambazo zimefaulisha wanafunzi hao ni sekondari ya wavulana Songea, sekondari ya wasichana Songea, Msamala, Londoni na sekondari ya Emmanuel Nchimbi.

Matokeo ya kidato cha sita kwa shule mbili ambazo sio za serikali yaani sekondari ya Beroya na Ruhuwiko yanaonesha kuwa, jumla ya wanafunzi wanne walipata daraja la kwanza na wanafunzi 98 wamepata daraja la pili.

Wanafunzi waliopata daraja la tatu katika shule hizo ni 105, daraja la nne wanafunzi walikuwa wanne na mwanafunzi mmoja tu alipata daraja sifuri.


Pamoja na mambo mengine Manispaa ya Songea ina jumla ya shule saba zenye kidato cha sita ambapo tano niza Serikali na mbili zinamilikiwa na watu binafsi.

No comments: