Thursday, October 26, 2017

KAYA MASKINI SONGEA WAWEZESHWA MILIONI 175


Baadhi ya wananchi waliopo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini katika Manispaa ya Songea wakipata huduma.
Na Albano Midelo,    
Songea.

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Euvuma, imeweza kuwasaidia wanufaika 4,881 waliopo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini katika halmashauri hiyo kwa kuwapatia shilingi milioni 175 ili ziweze kuwasaidia na hatimaye waweze kuondokana na umaskini.

Christopher Ngonyani ambaye ni Mratibu wa mfuko huo katika halmashauri hiyo alimweleza mwandishi wetu kuwa fedha hizo zimetolewa katika kipindi cha mwezi Septemba hadi Oktoba mwaka huu.

Alisema malipo hayo yamefanyika na kukamilika ndani ya wiki hii katika mitaa 53 ambayo ina wanufaika hao.


Ngonyani alibainisha kuwa kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi milioni 133 wamelipwa wanufaika 3,608 kwa njia ya fedha taslimu na shilingi zaidi ya milioni 42 wamelipwa wanufaika 1,273 kwa njia ya mitandao ya simu.

Alisema malengo waliyojiwekea ni kuhakikisha kwamba wanufaika wote wa TASAF wanaingizwa kwenye mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao huo kwa kuwa malipo yamekuwa yakilipwa moja kwa moja na TASAF kutoka makao makuu Dar es Salaam, badala ya fedha kutumwa katika halmashauri kitendo ambacho hutumia muda mrefu hadi kuwafikia walengwa.

Utafiti uliofanywa katika mitaa mbalimbali ambayo wanufaika hao wamelipwa kwa njia ya mtandao, umebaini kuwa mfumo huo umepata mafanikio makubwa baada ya wanufaika wengi kupata fedha zao kwa wakati, ingawa changamoto ilijitokeza kwa baadhi ya kampuni za simu kushindwa kuwalipa wanufaika kwa njia ya mtandao.

Manispaa ya Songea ni moja kati ya halmashauri 16 nchini zilizochaguliwa kufanya majaribio ya malipo kwa njia ya mtandao wa simu kwa wanufaika wa TASAF ili kuepukana na changamoto zilizokuwa zimejitokeza za  kutumia mfumo wa kulipwa fedha taslimu.


Hata hivyo mpango wa kunusuru kaya maskini hapa nchini umekuwa ukiendeshwa katika halmashauri 163 na kwamba mpango huo umezinufaisha kaya maskini zikiwemo zile ambazo awali zilikuwa zinapata mlo mmoja kwa siku ambapo hivi sasa wanaweza kupata milo mitatu kwa siku.

No comments: