Wednesday, October 25, 2017

SAKATA LA MSITU WA MBAMBI LAENDELEA KUMSAKAMA MKURUGENZI HALMASHAURI MJI WA MBINGA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli.
Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

SAKATA la tuhuma wizi wa mamilioni ya fedha za mradi wa uvunaji wa msitu wa Mbambi katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, limeibua sura mpya baada ya wananchi wa kata ya Matarawe mjini hapa kuitaka halmashauri hiyo iwalipe asilimia 10 ya fedha za mapato yaliyotokana na msitu huo.

Asilimia hiyo ya mapato wanayodai wananchi hao imeelezwa kuwa ni makubaliano yaliyofanywa katika vikao halali vilivyopita na kupitishwa na baraza la Madiwani wa halmashauri ya mji huo.

Walisema wanamshangaa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Robert Kadaso Mageni kwa kutosimamia kikamilifu fedha za msitu huo na kusababisha wizi huo ufanyike na wao kukosa sehemu ya mapato yao.


Hayo yalisemwa juzi na wananchi hao katika kikao cha kujadili maendeleo yao ya kata hiyo kilichofanyika katani humo ambacho kilikuwa na majadiliano pia ya ujenzi wa vibanda vya soko la kata ya Matarawe.

Mwenyekiti wa kata hiyo, Philibert Hyera alisema kuwa msimamo waliokuwa nao wanataka walipwe sehemu ya asilimia 10 iliyotokana na mapato ya fedha za uvunaji wa msitu wa Mbambi kwani wao ndio walioshiriki kwa miaka mingi kuutunza msitu huo.

“Sisi tunataka pia hata magogo ya miti na mbao zilizobakia kule msituni, halmashauri itupatie ili ziweze kutusaidia katika shughuli zetu za maendeleo ya kata”, alisisitiza Hyera.

Naye Diwani wa kata hiyo, Leonard Mshunju aliongeza kuwa maadhimio na michango yote iliyotolewa na wananchi wa kata yake atayafikisha kwenye kikao cha baraza la Madiwani kitakachoketi Novemba 27 mwaka huu ili kuweza kufikia muafaka na kufanyiwa utekelezaji.

Awali hivi karibuni kufuatia sakata hilo la uvunaji wa msitu huo, baraza la Madiwani la halmashauri hiyo lilitoa pendekezo lake la kumkataa Mkurugenzi huyo wa halmashauri hiyo, Mageni kwamba hawataki kufanya naye kazi tena wakimtuhumu ametafuna fedha za mauzo ya mbao zilizopasuliwa katika msitu huo na kulipotosha baraza kwa kutoa taarifa za uongo juu ya mapato yaliyotokana na uvunaji uliofanyika huko msituni.

Kufuatia upotoshaji huo anaotuhumiwa kulidanganya baraza hilo, anadaiwa kusababisha halmashauri iweze kupata hasara ya shilingi milioni 888,000,000 na kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli amchukulie hatua za kinidhamu ikiwemo ahamishwe haraka hawataki kufanya naye kazi.

Maamuzi hayo ya baraza hilo yalifikiwa baada ya Kamati maalum iliyoundwa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kutoa taarifa yake ya uchunguzi katika baraza la dharula lililoketi Novemba 20 mwaka huu, kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, ambapo baada ya kufanya uchunguzi wake waliweza kubaini mapungufu yaliyojitokeza katika shughuli hiyo ya uvunaji wa msitu wa Mbambi.

No comments: