Friday, October 6, 2017

WATUMISHI SONGEA WAPATA MAFUNZO YA KUANDAA BAJETI KWA MFUMO WA MTANDAO

Christopher Ngonyani mwezeshaji wa mafunzo ya kuandaa bajeti kwa mfumo wa mtandao akitoa elimu kwa watumishi wa halmashauri ya Manispaa ya Songea namna ya kutumia mfumo huo.
Watumishi wakiwa katika mafunzo ya mfumo wa kuandaa bajeti kwa njia ya kieletroniki. 
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WATUMISHI 49 waliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamepata mafunzo ya siku tano ya Mfumo wa kieletroniki ambayo yatapunguza gharama za uendeshaji katika maandalizi, uwasilishaji na utekelezaji wa mipango ya bajeti mpya katika shughuli mbalimbali za halmashauri.

Mafunzo hayo yamefunguliwa juzi na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa hiyo, Injinia Samwel Sanya katika ukumbi wa halmashauri hiyo uliopo mjini hapa.

Christopher Ngonyani ambaye ndiye mwezeshaji wa mafunzo hayo alisema kuwa mfumo huo mpya ambao umeanza kutumika rasmi hapa nchini kuanzia mwezi Septemba mwaka huu, utaweza kupunguza gharama za safari kwa Wakuu wa idara na wahasibu ndani ya halmashauri zote hapa nchini.


Ngonyani alisema kuwa kupitia mfumo huo mpya kila kitu katika mchakato wa bajeti kitafanyika katika halmashauri kwa njia ya mfumo wa kieletroniki, hivyo safari kwa Wakuu hao wa idara zitapunguzwa na kuondolewa.

Kwa mujibu wa Ngonyani, aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo Wakuu wa idara, vitengo na watumishi wengine wataanza kuandaa bajeti ya mwaka 2018/2019 kupitia mfumo huo mpya, ambapo utekelezaji wa maandalizi ya bajeti hiyo mpya unatarajia kuanza mwezi Oktoba mwaka huu.

Pamoja na mambo mengine, mfumo huo mpya ulizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Septemba 5 mwaka huu mjini Dodoma.
nayo.

No comments: