Thursday, October 26, 2017

WOFMAIZE YASHINDA ZABUNI YA KUKUSANYA USHURU SONGEA

Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji akisaini mikataba kati ya Manispaa hiyo na Kampuni ya WOFMAIZE kwa ajili ya kampuni hiyo kuanza kazi ya kukusanya ushuru wa shilingi milioni 610 baada ya kushinda zabuni. 
Na Albano Midelo,    
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imesaini mkataba wa ukusanyaji ushuru wa mazao wa shilingi milioni 610 na kampuni ya WOFMAIZE iliyopo hapa Songea.

Makubaliano ya kusaini mkataba huo yamekamilika Oktoba 24 mwaka huu katika Ofisi ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Hassan Mshaweji huku yakishuhudiwa na wawakilishi wa kampuni hiyo pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Songea Injinia Samwel Sanya.

Katika mikataba hiyo kampuni hiyo itahusika na ukusanyaji ushuru wa mazao ya vyakula vilivyosindikwa na visivyosindikwa katika maeneo ya SODECO, Manzese na maeneo mengine ya Manispaa hiyo.


Mkataba huo ni wa miezi tisa ambao unaanza mwezi Oktoba mwaka huu hadi Juni 30 mwaka 2018 ambapo kampuni ya WOFMAIZE italipwa asilimia ya makusanyo yote katika kipindi hicho ambayo ni sawa na zaidi ya milioni 90.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Mshaweji ameipongeza kampuni hiyo kwa kushinda zabuni ya ukusanyaji ushuru huo ambapo ameitaka kuzingatia masharti yaliyopo katika mkataba na kukusanya ushuru kwa uaminifu.

Mkurugenzi wa WOFMAIZE, Wofram Mlowe ameahidi kampuni yake kufanya kazi kwa uaminifu mkubwa ili kufikia malengo ya kukusanya milioni 610 au zaidi katika kipindi cha miezi tisa.

Kadhalika Manispaa hiyo imeamua kusaini makubaliano hayo kwa ajili ya ubinafsishaji wa vyanzo vya mapato katika kipindi cha mwaka 2017/2018 na lengo likiwa kukusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 100.

No comments: