Thursday, October 26, 2017

WANANCHI MBINGA WAITAKA SERIKALI KUWAJIBISHA WAHUSIKA UPOTEVU WA MAPATO MSITU WA MBAMBI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

BAADA ya taarifa ya Kamati maalum iliyofanya kazi ya kuchunguza uvunaji msitu wa Mbambi uliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, kuwasilisha taarifa ya kazi iliyofanya na kubaini hasara ya mapato ya shilingi milioni 800 ambayo ilibidi yapatikane kutokana na uvunaji huo, baadhi ya wananchi wamesema kuwa usimamizi wa kazi hiyo ungekuwa mzuri fedha hizo zingepatikana na kuweza kuboresha huduma muhimu katika hospitali ya wilaya ya Mbinga iliyopo mjini hapa.

Kadhalika walieleza kuwa hospitali hiyo ambayo hivi sasa baadhi ya majengo yake ni chakavu likiwemo jengo la upasuaji ambalo halijafanyiwa ukarabati kwa miaka mingi huku hali ya huduma ikiwa mbaya hivyo wanaiomba serikali kuchukua hatua ili kuweza kunusuru hali hiyo.

“Hata dawa za kuhudumia akina mama wajawazito pale wanapofikia hatua ya kujifungua wakati mwingine hazipatikani kwenye hii hospitali yetu na kusababisha baadhi yao kupoteza maisha lakini fedha hizi zingepatikana zingeweza kuhudumia jamii”, walisema.


Walisema kuwa fedha hizo zingeweza hata kutumika kununua majokofu ya kuhifadhia maiti katika jengo maalum lililopo katika hospitali hiyo ya wilaya ambalo limejengwa kwa miaka mingi na halina majokofu hayo huku maiti zikihifadhiwa katika mazingira magumu.

Hayo yalisemwa na wananchi hao jana kwa nyakati tofauti wakati walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari huku wakiipongeza Kamati maalum iliyopewa kazi ya kuchunguza ubadhirifu huo uliojitokeza kwenye uvunaji wa msitu wa Mbambi uliopo katika kata ya Matarawe mjini hapa.

Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao walisema kuwa baraza maalum la Madiwani ambalo liliketi Oktoba 20 mwaka huu na kupokea taarifa hiyo limetenda haki kwa wananchi wa Mbinga, kwani wanaimani kuwa ndani yake itakuwa na ukweli kwa asilimia nyingi hivyo Serikali wameitaka kusimamia hilo ili mwisho wa siku wahusika wanaotuhumiwa wachukuliwe hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

Pia walifafanua kuwa kuwepo kwa mikanganyiko ya sahihi katika mikataba ya uvunaji wa msitu huo na kutofuata sheria ya tangazo la Serikali GN namba 324 la Agosti 21 mwaka 2015, kuna kila sababu kwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, Robert Kadaso Mageni na watendaji wenzake wanaotuhumiwa kuhusika katika jambo hili kuchukuliwa hatua ili iweze kuwa fundisho kwa viongozi wengine wenye tabia kama hiyo.

“Haiwezekani leo hii Rais wetu alimuamini Mkurugenzi huyu na kumpatia majukumu ya kuongoza halmashauri yetu, halafu hata usimamizi wa mradi huu wa kuvuna msitu ameshindwa kusimamia kikamilifu badala yake imetokea hasara ambayo sasa ni aibu na inazorotesha maendeleo yetu”, walisema.

Katika hatua nyingine, kwa mujibu wa nakala ya taarifa ya uchunguzi wa msitu huo inaeleza pia Kamati maalum iliyofanya kazi hiyo ilibaini kwamba Afisa misitu wa halmashauri ya mji huo, David Hyera alikuwa anapokea fedha taslimu kutoka kwa wateja waliokuwa wananunua mbao na baadhi ya fedha zilikuwa hazipelekwi benki kwenye akaunti husika ya halmashauri.

Kamati hiyo inasema, utaratibu huo uliokuwa ukitumika ulikuwa unakiuka na kutofuata taratibu za uuzaji wa mali za Serikali ambazo zimeanishwa kwenye kanuni ya fedha za Serikali za Mitaa (LAFM) mwaka 2009 kifungu namba 45 na kifungu kidogo cha 3 kinachotaka mauzo ya mali za halmashauri zinapaswa kufanyika kwa njia ya mnada baada ya tangazo la mnada husika kufanyika.

Taarifa hiyo inaongeza pia, Kanuni za Serikali za Mitaa (Mamlaka za miji) (Maadili ya Madiwani) za mwaka 2000 kifungu cha 28(1) kinasema; “Pale ambapo afisa wa Serikali za Mitaa kwa makusudi au kwa uzembe atatoa taarifa za uongo au ushauri mbaya kwa halmashauri na kutokana na taarifa hizo au ushauri huo unafanywa na kutokana na uamuzi huo halmashauri inaingia katika hasara, afisa huyo atawajibishwa yeye mwenyewe au kwa pamoja kwa kulipa hasara iliyopatikana”, inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Vilevile uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa kanuni za fedha za Serikali za Mitaa mwaka 2009 kifungu cha 37(2) kinasema fedha zote zinazokusanywa na wakusanyaji mapato, zinatakiwa kuwasilishwa kwa mhasibu au benki kabla ya siku ya kazi kwisha au siku ya pili ya kazi, hivyo basi kama ilikuwa haifanyiki hivyo kuna kila sababu kwa mamlaka husika kuchukua hatua kwa wahusika wanaotuhumiwa.


Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Mageni alipohojiwa na waandishi wa habari alisema kuwa yeye hawezi kuzungumzia jambo lolote hivi sasa juu ya tuhuma hizo za upotevu wa mapato ya uvunaji msitu wa Mbambi kama zina ukweli au la.

No comments: